Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

28 Oktoba 2022

19:28:19
1318109

Somalia yataka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuharakisha kuiunga

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ameitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuharakisha kuiunga nchi yake katika jumuiya ya kikanda.

Taarifa hiyo imetolewa na makao makuu ya EAC jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania na kumnukuu Rais Mohamud akitoa mwito huo wakati wa ziara ya kwanza ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Peter Mathuki katika mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu.

Mohamud amesema suala la nchi yake kujiunga na EAC limekuwa ni ndoto iliyochelewa kuaguliwa. Amemtaka Katibu Mkuu huyo wa EAC kuharakisha mchakato wa udahili ili Somalia iwe mwanachama wa 8 wa EAC. EAC ni jumuiya ya kikanda ya kiserikali.

Wanachama wake ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Rais Mohamud amesema: "Somalia ni mali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hakuna nchi kati ya nchi wanachama wa EAC ambayo haihusiani na biashara na Somalia, na uhusiano uliopo wa kihistoria ni pamoja na lugha na utamaduni."

Pia amemwambia Katibu Mkuu huyo wa EAC kuwa, Somalia inajitahidi bila kuchoka kuondoa changamoto zote za kiusalama kwa kuungwa mkono na baadhi ya nchi wanachama wa EAC.

Amesisitizia msimamo wa kimkakati wa Somalia, akibainisha kuwa EAC itafaidika kwa kiasi kikubwa kupitia ongezeko la usafirishaji wa bidhaa, huduma na ongezeko la idadi ya watu katika kambi hiyo pamoja na kupanua biashara ya ndani ya kanda.

Amesema, Somalia inaweza kuzisaidia sana nchi za jumuiya ya EAC ikiwemo utajiri wake wa baharini. Kwa upande wake, Mathuki amepongeza nia ya Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na amemhakikishia Rais Mohamud kuwa sekretarieti ya EAC itafanya kuwa ni ajenda yake mchakato mzima wa kujiunga Somalia na jumuiya hiyo.

342/