Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

28 Oktoba 2022

19:28:46
1318110

Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Tutalipiza kisasi cha damu ya mashahidi wa jinai ya Shiraz

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amelaani vikali shambulio la kigaidi katika Haram takatifu ya Ahmad bin Musa (as) huko katika mji wa Shiraz na kusisitiza kwamba, taifa hili litalipa kisasi cha damu ya mashahidi waliouawa kinyama na kidhulma katika tukio hilo.

Hujjatul Islam Muhammad Javad Haj Ali Akbari amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya kimaanawi na kisiasa ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran ambapo sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao wapendwa waliouawa katika shambulio la kigaidi dhidi ya Haram ya Shah Cheragh amesisitiza kuwa, taifa hili litalipa kisasi cha damu ya mashahidi hao kwa Uistikbari wa dunia uliosababiisha kutokea jinai hiyo.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema, kwa hakika ni tukio chungu na la kuumiza moyo mno kuona watu wasio na hatia ambao wamekwenda kufanya ziara na ibada wakiuawa kinyama namna ile kwa kumiminiwa risasi.

Wakati huo huo, wananchi wa jiji la Tehran na miji yote ya Iran, leo baada ya Swala ya Ijumaa, wamefanya maandamano makubwa ya nchi nzima kulaani shambulio la kigaidi lililotokea juzi Jumatano katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh ya mjini Shiraz, kusini magharibi mwa Iran.  Waandamanaji hao wenye hasira wamelaani ugaidi huo na kutoa wito wa kushughulikiwa wale wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine katika jinai hiyo ya kinyama. 

Watu wasiopungua 15 waliuawa huku 27 wakijeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi la juzi Jumatano katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh mjini Shiraz, katika mkoa wa Fars wa kusini magharibi mwa Iran. Genge la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika na jinai hiyo.

Hadi hivi sasa nchi mbalimbali duniani zimeshatoa mkono wa pole kufuatia shambulio hilo la kigaidi. Miongoni mwa nchi hizo ni Russia, China, Uturuki, Pakistan, Armenia, Jamhuri ya Azerbaijan, Misri, Imarati, Venezuela, Oman, Syria, Iraq, Finland, Umoja wa Mataifa, harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Kataib Hizbullah ya Iraq, Ansarullah ya Yemen n.k, ambapo zimetoa mkono wa rambirambi kwa serikali na taifa la Iran kufuatia jinai hiyo.

342/