Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

28 Oktoba 2022

19:31:05
1318114

Misri, Oman na Imarati zalaani shambulio la kigaidi katika haram tukufu ya mjini Shiraz, Iran

Nchi za Oman, Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri zimelaani shambulio la kigaidi lililofanyika kwenye haram tukufu ya Shah Cheragh mjini Shiraz, kusini magharibi mwa Iran.

Shirika la habari la Mehr limeripoti habari huyo na kunukuu taarifa za nchi mbili Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu pamoja na mazungumzo ya simu ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Oman kwa ajili ya kulaani shambulio hilo la kigaidi na kikatili ambalo genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman imelaani shambulizi hilo la kigaidi na kusema kuwa, Muscat inapinga jinai na ugaidi wa aina yoyote ile. 

Sayyid Badr bin Hamad al Busaidi amezungumza kwa simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Iran, Hossein Amir-Abdolahian na kumpa mkono wa pole kutoka kwa Sultan Haitham bin Tariq kwa ajili ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa serikali na wananchi wa Iran kufuatia jinai hiyo ya kutisha iliyotokea mjini Shiraz. 

Amma katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje wa Imarati imesema, Abudhabi inalaani vikali shambulio hilo la kigaidi lililopelekea kuuawa na kujeruhiwa makumi ya watu wasio na hatia. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Muungano wa Falme za Kiarabu, mbali na kulaani vikali jinai hiyo inatangaza wazi kuwa inapinga matumizi yoyote ya mabavu na ugaidi yenye shabaha ya kuvuruga usalama na utulivu wa nchi na ambao unakwenda kinyuma na matukufu na misingi ya kibinadamu.

Vile vile Muungano wa Falme za Kiarabu umetoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi wa Iran na familia za wahanga wa shambulio hilo la kigaidi.

Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri nayo imetoa taarifa ya kulaani shambulio hilo la kigaidi katika haram tukufu ya Shah Cherag mjini Shiraz, Iran.

Katika taarifa yake hiyo, Misri imetoa mkono wa pole kwa familia za watu waliouawa na kujeruhiwa kwenye jinai hiyo. Pia imesema kuna wajibu kwa jamii ya kimataifa kuwa na kauli moja ya kulaani na kupambana na aina zote za vitendo vya kigaidi.

Watu wasiopungua 15 wameuawa huku 27 wakijeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi la juzi Jumatano yapata saa 12 kasorobo kwa majira ya hapa Iran katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh mjini Shiraz, katika mkoa wa Fars wa kusini magharibi mwa Iran.

Hadi hivi sasa nchi mbalimbali duniani zimeshatoa mkono wao wa pole kufuatia shambulio hilo la kigaidi. Miongoni mwa nchi hizo ni Russia, China, Uturuki, Pakistan, Armenia, Jamhuri ya Azerbaijan, Misri, Imarati, Venezuela, Oman, Syria, Iraq, Finland na Umoja wa Mataifa.

Leo kona zote za Iran kutafanyika maandamano makubwa baada ya Sala ya Ijumaa kulaani jinai hiyo.