Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

28 Oktoba 2022

19:31:45
1318115

Serikali ya Uganda yaandamwa huku maambukizo ya Ebola yakisambaa zaidi

Serikali ya Uganda inakabiliwa na mashinikizo ikilaumiwa kwamba, haikuchukua hatua za maana na za haraka kwa ajili ya kukabiliana na maambukizo ya ugonjwa wa Ebola.

Wataalamu wa afya nchini Uganda wanasema kuwa, serikali ya nchi hiyo inabeba dhima ya kusambaa Ebola nchini humo kwani haikuchukua hatua za haraka kukabiliana na maambukizo ya ugonjwa huo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wakati awali kulikuwa na taarifa za kuenea ugonjwa huo katika mji mkuu Kampala serikali iliendelea kusisitiza kwamba, hakuna maambukizo katika mjii huo.

Watalaamu hao wanasema kuwa, uzembe wa serikali katika kuchukua hatua za haraka umechangia pakubwa maradhi hayo kuenea hasa katika jiiji la Kampala.

Lawama hizo zinatolewa baada ya maafisa wa mji mkuu Kampala kutangaza kuwa, watoto sita wa familia moja ya mji huo wamepata maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.

Watoto hao sita ndugu wa familia moja walipata maambukizi baada ya ndugu yao aliyetoka katika moja ya wilaya zilizoathiriwa zaidi kwenda kuishi nao, na baadaye kufariki dunia.

Maafisa wa afya wakimchukua mgonjwa wa Ebola

 

Hayo yanajiri wakati ambao, shirika la juu zaidi la afya ya umma barani Afrika (Afrika CDC) limetangaza leo Alhamisi kwamba mlipuko wa Ebola nchini Uganda bado unadhibitiwa, licha ya kuongezeka kwa kesi za maambukizi ya ugonjwa huo hadi katika mji mkuu, Kampala.

Virusi vinavyoenea nchini Uganda ni aina ya Ebola ya Sudan, ambayo hakujapatikana chanjo iliyothibitishwa ya kukabiliana navyo, tofauti na aina ya kawaida ya Zaire iliyoonekana wakati wa milipuko ya hivi karibuni katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

342/