Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

28 Oktoba 2022

19:33:56
1318118

Somalia yataka isaidiwe na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarisha mifumo yake ya mahakama

Jaji Mkuu wa Somalia amewasilisha ombi maalumu Kwa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuisaidia Somalia kuimarisha mifumo ya kimahakama ambayo imeathiriwa vibaya na vita hatua itakayoharakisha mchakato unaoendelea wa nchi hiyo wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Yusuph Bashe Mohamed Jaji Mkuu wa Somalia amewasilisha ombi hilo katika Mkutano wa pili wa Majaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoendelea katika jiji la Kampala nchini Uganda ukishirikisha pia majaji wa mahakama za ndani na nje ya nchi za jumuiya hiyo.

Amesema mifumo ya mahakama ikiimarika itaongeza upatikanaji wa haki suala ambalo litawawezesha wananchi kuongeza imani kwa serikali na kwamba wana imani ya kupata msaada kutoka katika jumuiya hiyo.

Suala hilo limezungumziwa pia na baadhi ya majaji akiwemo Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki Nestor Kayobera ambaye amesema licha ya kuwa ni jambo jema linahitaji kupitia katika ngazi zinazohusika. 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ameitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuharakisha kuiunga nchi yake katika jumuiya ya kikanda.

Mohamud amesema suala la nchi yake kujiunga na EAC limekuwa ni ndoto iliyochelewa kuaguliwa, hivyo amemtaka Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuharakisha mchakato wa udahili ili Somalia iwe mwanachama wa 8 wa EAC.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ni taasisi ya kikanda ya kiserikali na mpaka sasa ina jumla ya wanachama saba ambao ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

342/