Main Title

source : Parstoday
Jumapili

30 Oktoba 2022

19:36:21
1318883

Maelfu ya Wairaq wamekimbia nchi yao katika kipindi cha miezi 10 iliyopita

Mkuu wa Kamisheni ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq na eneo la Kurdistan la nchi hiyoi jana (Jumamosi) alifichua kuwa, katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, karibu Wairaqi 75,000 wamekimbilia nje ya nchi hiyo.

Shirika la habari la Shafaq News limemnukuu Amanj Abdullah Saeed akisema hayo na kuongeza kuwa, tangu mwanzoni mwa mwezi Januari 2022 hadi mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba, karibu wananchi 75,000 wa Iraq wamekimbilia nchi nyingine huku zaidi ya 28,000 kati yao wakiwa wametoka kwenye eneo la Kurdistan ya Iraq.

Amma kuhusu watu waliopoteza maisha katika harakati hizo za ukimbizi, Saeed amesema, katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, karibu watu 38 wamekufa maji na wengine 28 hawajulikani walipo. Pia amesema, idadi nyingine kubwa ya raia wa Iraq wako katika jela na korokoro za nchi nyingine. 

Amezungumzia taathira mbaya za vita vya Ukraine katika ongezeko la wakimbizi hao na kusema kuwa, hali ya wakimbizi wa Iraq barani Ulaya inazidi kuwa mbaya, siku baada ya siku.

Amma kuhusu hatua ya Uingereza ya kukataa kupokea wakimbizi anapokuwa mtu mmoja mmoja mpaka wawe ni familia amesema, ijapokuwa uamuzi huo haujaanza kutekelezwa lakini athari zake kwa wakimbizi vijana ni mbaya sana.

Mkuu huyo wa UNHCR nchini Iraq na eneo la Kurdistan la nchi hiyo amezungumzia pia uhakika kwamba suala la wakimbizi linatumiwa kama turufu ya mashinikizo ya kisiasa katika baadhi ya nchi na kusisitiza kuwa, wakimbizi ni sehemu dhaifu zaidi katika mazungumzo na hatua za kimataifa.

342/