Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

31 Oktoba 2022

19:44:50
1319241

Rwanda 'yasikitishwa' na kufukuzwa kwa balozi wake na DR Congo

Serikali ya Rwanda siku ya Jumapili imetangaza kusikitishwa na uamuzi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ya kumfukuza balozi wake huku hali ya wasiwasi ikiongezeka kuhusu waasi wa M23 wanaopambana na wanajeshi wa serikali mashariki mwa DRC.

Vincent Karega, ambaye aliteuliwa kuwa balozi wa Rwanda mjini Kinshasa mwaka 2019, Jumamosi alipewa saa 48 kuondoka nchini humo kwa madai kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa Kongo wa M23 kufuatia mapigano mapya na wanajeshi wa serikali katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Taarifa ya msemaji wa serikali ilisema Rwanda inasikitishwa na uamuzi wa serikali ya DRC kumfukuza Balozi wa Rwanda Vincent Karega.

Kufukuzwa kwa mjumbe huyo kulikuja siku ambayo wapiganaji wa M23 waliteka miji ya Kiwanja na Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Taarifa hiyo imesema, "vikosi vya usalama vya Rwanda kwenye mpaka wetu na DRC vinaendelea kuwa macho, huku tukiendelea kufuatilia kuongezeka uchochezi wa Kongo."

Mwezi Mei pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kongo ilimwita Karega ili kumuhoji kuhusu madai hayo kuhusu waasi wa M23.

Rwanda ilikariri wasiwasi wake juu ya kile ilichokiita kuendelea kushirikiana kati ya wanajeshi wa Kongo na waasi wa Rwanda wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, wenye makao yake nchini Kongo.

Rwanda pia ilishutumu kile ilichosema ni "majaribio ya kulenga eneo la mpaka kwa silaha nzito, pamoja na maneno ya kupinga Rwanda yanayotangazwa na maafisa wa DRC."

Pia ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kuhusu madai ya kuendelea kwa matamshi ya chuki, uchochezi wa hadharani, na unyanyasaji wa dhuluma dhidi ya Wanyarwanda na jamii zinazozungumza Kinyarwanda nchini DR Congo.

DR Congo imeendelea kuishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda inayakanusha.

 

342/