Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

31 Oktoba 2022

19:50:20
1319250

Matokeo ya Sensa: Idadi ya watu Tanzania yafikia milioni 61.74 + SAUTI

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametangaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti mwaka huu akisema kuwa idadi ya Watanzania ni milioni 61,741,120.

Akitangaza matokeo hayo, Rais Samia amesema, kati yao wanawake ni milioni 31.6 sawa na asilimia 51 na wanaume milioni 30.53 sawa na asilimia 49 ya watu wote.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya sensa, kati ya hao Watanzania milioni 59.8 wako Tanzania Bara na watu milioni 1.8 wako katika visiwa vya Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kadhalika amesema kuwa, mkoa wa Dar es Salaam ndio unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu nchini humo ambao ni milioni 5.3 sawa na asilimia saba na kufuatiwa na Mwanza watu milioni 3.6 sawa na asilimia sita. 

Akiendelea kuchambua matokeo hayo ya sensa, Rais Samia  Suluhu Hassan amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka 10 kuna ongezeko la watu milioni 16.8 sawa na asilimia 3.2.

“Miaka kumi iliyopita Tanzania ilikuwa na watu 44, 928, 923 hii inaonyesha kumekuwapi na ongezeko la watu milioni 16,812,197 sawa na ongezeko la asilimia 3.2 ya waliokuwepo kati ya mwaka 2012 na mwaka 2022.

“Tanzania Zanzibar, Idadi ya watu imeongezeka kutoka 1,303,569 mwaka 2012 hadi watu 1, 889,773 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 3.7” amesema.

342/