Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

5 Novemba 2022

21:09:25
1320650

Uchunguzi: Mtazamo chanya wa Waafrika kuhusiana na China unazidi kuongezeka

Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na Taasisi ya You-Gov Cambridge unaonyesha kuwa, idadi ya Waafrika wenye mtazamo chanya kuhusiana na China inaendelea kuongezeka.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na Taasisi ya You-Gov Cambridge katika miezi ya Agosti na Septemba kwa watu elfu moja katika nchi 25, zikiwemo nchi tatu kubwa za Afrika ikiwa ni pamoja na Nigeria, Kenya na Afrika Kusini unaonyesha kuwa, mtazamo chanya wa watu wa bara la Afrika kuhusiana na China unaendelea kuongezeka.

Kulingana na uchunguzi huo wa maoni ya You-Gov, China ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa bara la Afrika na inachukuliwa kuwa ni nguvu chanya katika nchi za bara hilo.

Nchini Afrika Kusini, asilimia 61 ya waliohojiwa katika zoezi hilo la uchunguzi wa maoni waliitaja China kama nchi yenye nafasi na mchango athirifu duniani. Kwa upande wa Kenya, wenye mtazamo huo wameripotiwa kuwa ni asilimia 82; na asilimia 83 ya waliohojiwa nchini Nigeria wanaitakidi hivyo pia.

Mkutano wa China na nchi za Afrika

Lakini mbali na hilo, kuhusu kuzipatia silaha za kivita nchi nyingine duniani katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na vilevile kuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo pamoja na kujihusisha na hujuma za kimtandao na ujasusi, Waafrika wameibebesha Marekani dhima ya vitendo hivyo na kuilaumu pia nchi hiyo.

Wakati huohuo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian amesema, "matokeo ya uchunguzi huu wa maoni kwa mara nyingine yameonyesha kuwa ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika utakuwa na manufaa mengi kwa watu wa bara hilo."

Mbali na hayo, wakati Rais Xi Jinping wa China alipohutubia mkutano wa ishirini wa taifa wa Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo alisema, China inadhamini maslahi ya pamoja ya nchi zinazostawi na itaufanya bora zaidi siku baada ya siku uhusiano wake na nchi hizo.../

342/