Main Title

source : Parstoday
Jumapili

6 Novemba 2022

20:32:33
1320967

Iran na Zimbabwe zatathmini njia za kuimarisha uhusiano wao

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe hapa mjini Tehran, na kujadili mikakati na njia za kupanua na kuboresha uhusiano wa pande mbili wa nchi hizi mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian ametilia mkazo suala la kufanyika mkutano wa Kamisheni ya Pamoja ya Uchumi ya Iran na Zimbabwe, kwa shabaha ya kupiga jeki ushirikiano wa Tehran na Harare.

Aidha Amir-Abdollahian ametoa mwito wa kutumia fursa na uwezo wa nchi mbili hizi kuboresha uhusiano na ushirikiano wa mataifa haya katika nyuga mbalimbali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, David Musabayana, pambizoni mwa mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Kundi la marafiki watetezi wa Hati ya Umoja wa Mataifa unaofanyika hapa Tehran.

Mkutano wa kwanza wa kimataifa wa kundi la marafiki watetezi wa Hati ya UN ulianza jana mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na manaibu mawaziri wa mambo ya nje, mabalozi, wawakilishi na wajumbe maalum wa marais wa nchi wanachama wa kundi hilo.

Kundi la Marafiki wa Hati ya Umoja wa Mataifa liliundwa mwaka 2021 kwa lengo la kulinda, kukuza na kutetea ubora na itibari ya Hati ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikisha nchi 19, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Washiriki wa mkutano huo wakiwemo manaibu mawaziri wa mambo ya nje wa Algeria, Angola, Belarus, Bolivia, Cambodia, China, Cuba, Korea Kaskazini, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Laos, Nicaragua, Palestina, Russia, Saint Vincent na Grenadines, Syria, Venezuela. na Zimbabwe, wamebadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya kimataifa, sanjari na kulaani ubeberu na uchukuaji wa maamuzi wa upande mmoja.

342/