Main Title

source : Parstoday
Jumatano

9 Novemba 2022

18:21:13
1321765

Utafiti: Theluthi moja ya Wazungu wamenyanyaswa kingono wakati wa masomo vyuoni

Uchunguzi uliofanyika barani Ulaya uliochapishwa Jumatatu wiki hii umeonyesha kwamba karibu thuluthi moja ya wanafunzi au wafanyakazi katika vyuo vikuu wamepitia aina fulani ya unyanyasaji wa kingono.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Leibniz ya Sayansi ya Jamii huko Cologne, Ujerumani, karibu thuluthi moja ya waliohojiwa wamenyanyaswa kingono wakiwa masomoni au kazini, asilimia 6 waliripoti kuathiriwa na unyanyasaji wa kimwili, na asilimia 3 kwa unyanyasaji wa kijinsia.

Taasisi hiyo ilifanya utafiti kwa kushirikiana na washirika wake wa Ulaya, ndani ya mfumo wa mradi wa Umoja wa Ulaya "UNI SAFE" – ili kukomesha unyanyasaji wa kijinsia - katika vyuo vikuu vya Ulaya na taasisi za utafiti.

Kwa ujumla, 62% ya wale waliohojiwa walisema wamepitia kwa uchache aina moja ya unyanyasaji wa kijamii katika vyuo vikuu au taasisi zao.

Dk. Anki Lipinski wa Taasisi ya Leibniz ya Sayansi ya Jamii amesema: "Ukatili wa kijinsia ni tatizo la kimfumo ambalo linaathiri taasisi za kisayansi, kama ilivyo katika sehemu nyingine za jamii".

Kulingana na utafiti huo, wanawake wameathirika zaidi kuliko wanaume katika takriban aina zote za ukatili – isipokuwa katika ukatili wa kimwili, ambao wanaume waliripoti kunyanyaswa zaidi kuliko wanawake.

Utafiti huo umewashirikisha wafanyakazi na wanafunzi kutoka vyuo vikuu 46 na taasisi za utafiti nchini Ujerumani na nchi nyingine 14 za Ulaya kuanzia Januari hadi Mei 2022.

342/