Main Title

source : Parstoday
Jumatano

9 Novemba 2022

18:21:41
1321766

Marubani wa Kenya Airways wasitisha mgomo, waanza kazi

Marubani wa Kampuni ya ndege ya Kenya, Kenya Airways mapema leo wamerejea kazini baada ya muungano wao (Kalpa), kusitisha mgomo uliovuruga safari za ndege kwa siku kadhaa.

Zaidi ya wasafiri 15,000 wameathiriwa na mgomo huo uliosimamisha safari zaidi ya 53 za ndani na nje ya nchi, kutokana na mgomo huo ulioanza Jumamosi iliyopita, huku wahudumu wengine wa shirika hilo na wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini Kenya wakijiunga na mgomo huo.

Marubani walianza kazi leo alfajiri saa kumi mbili muda ulioagizwa na mahaka ya kazi.

Jaji wa mahakama ya Kenya alikuwa amesema jana Jumanne kwamba wanapaswa kurejea kazini ‘’bila masharti’’ wakati wakisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu iwapo mgomo ulikuwa wa kisheria au la.

Jaji Anna Mwaure pia alisema kuwa Kenya Airways inapaswa kuwaruhusu marubani kufanya kazi yao "bila unyanyaso au vitisho".

Marubani wamekuwa wakipinga hatua ya muaji wao kuondoa michango yao kwenye mfuko wa akiba ya uzeeni.

Awali Chama cha Marubani wa Mashirika ya Ndege ya Kenya (KALPA) kilisema kuwa, wanachama wao hawatarejea kazini hadi matakwa yao yatimizwe.

Usimamizi wa Kenya Airways unasema mgomo huo ulikuwa hujuma kwa uchumi wa Kenya, na utalisababishia shirika hilo hasara ya Shilingi milioni 300 za Kenya kila siku.

Kenya Airways inayomilikiwa na serikali ya Kenya ni mojawapo ya mashirika makubwa ya usafiri wa anga barani Afrika, ikiunganisha miji mingi katika mabara ya Afrika, Asia na Ulaya na hivyo mgomo huo umesababisha adha na usumbufu mkubwa kwa wasafiri wengi.

342/