Main Title

source : Parstoday
Jumatano

9 Novemba 2022

18:22:21
1321767

Russia yazishutumu nchi za Magharibi kwa kuvuruga utulivu wa kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amezishutumu na kuzilaumu nchi za Magharibi kwa kuvuruga utulivu wa kimataifa.

Shirika la habari la "RIA Novosti" limeripoti habari hiyo na kumnukuu Sergey Lavrov akitoa lawama hizo jana Jumanne wakati akihutubia mkutano wa kimataifa uliobeba kaulimbiu ya "Matatizo ya Kweli ya Usalama wa Kimataifa katika Hali ya Ukosefu wa Utulivu wa Jeopolitiki" na kusisitiza kuwa, hali ya usalama duniani leo ni tete mno.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinavuruga usalama wa nchi zote dunia kwa shabaha ya kulinda ubeberu wao.

Vile vile amesema,  maana mpya ya ukoloni duniani ambayo inaenezwa na Marekani na waitifaki wake hivi sasa, inapingwa na nchi nyingi ambazo zinapigania kuweko mfumo wa kiuadilifu, wa demokrasia ya kweli na wa mahusiano ya kiuadilifu, ya usawa na ya kuheshimiana duniani. 

Aidha amesisitiza kuwa, Russia inapigania kwa dhati kupatikana mfumo huo mpya wa dunia ambao utakuwa na uhuru wa kweli wa kisiasa, kijamii na kiuchumi na ambao utatoa fursa pana za ustawi na maendeleo kwa mataifa yote duniani bila ya ubaguzi wala kushinikizwa taifa lolote.

Kabla ya hapo pia, waziri huyo wa mambo ya nje wa Russia alikuwa ameilaumu vikali Marekani na kusema kuwa. lengo la Washington ni kuzidhoofisha nchi za Ulaya kiuchumi na kijeshi. Amesema, nchi zilizopata madhara makubwa zaidi katika vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia ni za barani Ulaya suala ambalo Marekani inalitumia kwa manufaa yake binafsi.

342/