Main Title

source : Parstoday
Jumatano

9 Novemba 2022

18:23:44
1321769

Sisitizo jingine la Marekani la kuunga mkono vurugu na machafuko nchini Iran

Ned Price, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ameendelea kuunga mkono vurugu na machafuko nchini Iran na kukana kabisa kuhusika nchi yake katika vurugu hizo.

Price amesema kuhusiana na madai ya Rais Joe Biden wa Marekani na matamshi yake ya wazi ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran ambayo yamekabiliwa na ulegezaji msimamo wa White House kwamba, alichokiashiria Biden ni hisia ambayo sisi tulikuwa nayo tangu mwanzoni mwa malalamiko ya Wairan wanaoandamana yaani hisia ya kuwa pamoja na waandamanaji hao.

Afisa huyu wa ngazi za juu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekanii amekiri kwa kusema: Sisi tangu katika siku za awali tulitangaza himaya na uungaji mkono wetu kwa maandamano ya wananchi wa Iran. Hata hivyo afisa huyo amekana kabisa kuhusika Marekani katika vurugu na machafuko ya hivi karibuni hapa nchini Iran yaliyoibuka yakitumia kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini.

Kadhalika amekana kuweko mkono kutoka nje katika machafuko ya Iran na kueleza kwamba, nafasi ya Marekani katika hili ni kuwataka wale wanaowakandamiza wananchi, wanaoamiliana vibaya na wananchi na kuwakatia mawasiliano ya intaneti wawajibike. 

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani amedai kuwa, Iran inapenda kuhusisha machafuko hayo na serikali ya Marekani ili kwa njia hiyo iweze kutoa lawama dhidi ya Washington.

John Bolton, aliiyekuwa mshauri wa usalama wa taifa katika serikali ya Rais mtata Donald Trump daima alikuwa na utendaji wa chuki na hasama na kutaka vita na Iran. Bolton sambamba na kuonyesha matumainii ya kubadilishwa mfumo wa utawala nchini Iran amesema kuwa, mrengo wa upinzani nchini Iran hivi sasa umo katika hatua ya kubeba silaha.

Sisitizo jingine la Marekani la kuunga mkono waziwazi machafuko na vurugu nchini Iran ni katika fremu ya siasa za Washington za kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine na ni katika sifa kuu za sera za kigeni za utawala wa Marekani.

Kuibuka machafuko ya hivi karibuni nchini Iran kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini kwa mara nyingine kumeifanya Marekani kuliangalia hilo kama fursa ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na wakati huo huo kuchochea vurugu na machafuko hayo kadiri inavyoweza.

Marekani imetoa ahadi ya kuondoa vikwazo vya Intaneti ili kwa njia hiyo ichochee zaidi na kupanua wigo wa vurugu hizo. Tangu Rais Joe Biden aingie madarakani nchini Marekani ameweka kando nara na kaulimbiu alizokuwa akitoa katika kampeni za uchaguzi na badala yake ameendeleza siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran na kila baada ya muda hutangaza vikwazo vipya dhidi ya taifa hili.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Hivi sasa Marekani imeweka kando mazungumzo ya nyuklia ya Vienna kwa kisingizio cha kuibuka ghasia na machafuko nchini Iran na kuamua kuwa pamoja na wapinzani wachache ambao wakitumia kisingizo cha kifo cha Mahsa Amini wamefanya uharibifu mkubwa wa mali za watu na za umma.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi ya hivi karibuni ya Joe Biden pale alipoandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter:

Bwana Biden acha utendaji wa kinafiki, wa ria na kujionyesha na kuunga mkono kundi la kigaidi la Daesh. White House ambayo imekuwa ikieneza utumiaji mabavu na mauaji, katika machafuko ya hivi karibuni ya Iran imekuwa ikifanya hayo sambamba na juhudi za kufikiwa makubaliano ya nyuklia.

Akihutubia hivi karibuni Bide aliapa kuhusu kile alitaja kuwa "kuikomboa" Iran na kusema waibua ghasia za hivi majuzi nchini Iran watafanikiwa ‘kujikomboa’ hivi karibuni. Biden ambaye hata vyombo vya habari vya Marekani vinatilia shaka uzima wake wa kiakili alisema kama ninavyonukuu: "Msiwe na wasiwasi, sisi tutaikomboa Iran. Waandamanaji hivi karibuni watafanikiwa kuwa huru". 

Tangu kuanza fujo hapa Iran siyo tu kwamba, Marekani imeonyesha misimamo ya kuingiliai masuala ya ndani ya taifa hili, bali imewawekea vikwazo viongozi na idara kadha za Iran. 

Rais Ebrahim Raeisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba kuwauliza viongozi wa Marekani swali hili kwamba, wanataka kupata ibra na funzo mara ngapi kutoka kwa Iran na Wairani na kwa nini hawajifunzi kutona ana makosa? Anasema kuwa: Wamarekani walidhani kwamba, wangeweza kutekeleza kwa Iran mpango uleule mchafu walioutekeleza kwa mataifa kama Syria, Libya na baadhi ya nchi za eneo, lakini hizo zilikuwa ndoto za alinachana na fikra batili.

Marekani ikiwa kinara wa kambi ya Magharibi siyo tu kuanzia kipindi cha uongozi wa Donald Trump iliamua kuchukua mkondo wa utekelezaji wa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa, uchochea machafuko ya kijamii na mashinikizo ya kiuchumi, bali kila baada ya muda imekuwa ikiingilia masuala ya ndani ya Iran ikitumia visingizo mbalimbali kama machafuko ya kulalamikia kupanda bei ya mafuta yaliyoibuka miaka mitatu iliyopita au vurugu za kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais za 2009 ambapo hufanya kila iwezalo kuwachochea na kuwaunga mkono watu wachache wanaofanya vurugu na kuharibu mali za watu na za umma.

Nukta muhimu na ya kuzingatia ni hii kwamba, kwa zaidi ya miaka 40 sasa ambapo Marekani imekuwa ikiiwekea vikwazo Iran na kutekeleza mpango wa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya wananchi wa Iran, lakini wakati huo huo imekuwa ikidai kwamba, inawaonea huruma mno wananchi wa Iran, madai ambayo bila shaka ni kioja na kichekesho hasa kwa kuzingatia kwamba, vikwazo vya Washington vimekuwa vikiwaathiri moja kwa moja wananchi wa taifa hili.