Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Novemba 2022

20:38:10
1322189

Rais Xi ameliamuru Jeshi la China kuzingatia 'maandalizi ya vita'

Rais Xi Jinping wa China ameliambia jeshi la nchi hiyo "kuelekeza nguvu zake zote kwenye mapigano" katika kujiandaa kwa ajili ya vita, huku kukiwa na taharuki zinazozidi kushadidi katika uhusiano wa China na Marekani kuhusu kisiwa cha Taipei cha China.

Rais Xi ameyasema hayo alipotembelea kamandi moja ya jeshi na kuongeza kuwa jeshi lazima "lijiimarishe kikamilifu  katika mafunzo ya kijeshi ili kujitayarisha kwa ajili ya vita.”

"Elekezeni nguvu zenu zote katika kupigana, fanyeni kazi kwa bidii katika kupigana na kuboresha uwezo wa kuwawezesha  kushinda," rais wa China alinukuliwa akisema.

Aidha kiongozi huyo wa China amesema, “Jeshi lazima pia "litetee mamlaka ya kujitawala na usalama wa taifa" kwani China inakabiliwa na hali ya usalama "isiyo na utulivu na isiyo na uhakika."

Rais Xi mwezi uliopita aliikosoa Marekani kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na uungaji mkono wake unaozidi kuwa wazi kwa Taipei katika mkutano wa 20 wa Chama cha Kikomunisti mjini Beijing. Rais wa China alisema "uingiliaji wa kigeni" umezidisha mvutano katika kadhia ya Taiwan. Katika hotuba yake Rais Xi alitoa onyo kali kwa kusema, "Hatutawahi kuahidi kutotumia nguvu za kijeshi."

Mnamo Septemba, China iliwasilisha "malalmiko makali" kwa Washington baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kusema kuwa vikosi vya nchi hiyo vitailinda Taiwan ikiwa kuna shambulio la China.

China inachukulia Taipei kama mkoa uliojitenga ambao unapaswa kuunganishwa tena na China chini ya sera inayotambuliwa kimataifa ya China Moja. Ni nchi chache sana duniani zinazotambua uhuru wa Taipei ikiwa ni pamoja na Marekani.

Uhusiano kati ya China na Marekani umedorora katika miaka ya hivi karibuni, huku mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani yakigongana kuhusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Taipei ya China.

342/