Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Novemba 2022

20:41:58
1322194

Iran yasisitiza sera zake za kuwa na uhusiano na ujirani mwema na majirani zake.

Nasser Kanaani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku akijibu madai ya hivi karibuni ya Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan kuhusiana na eti uungaji mkono wa Iran kwa Armenia, amesisitiza kuwa sera kuu za Iran zimejengeka katika msingi wa kuwa na ujirani mwema na kupanua mahusiano na majirani wake wote na kuwa kuimarisha uhusiano na mmoja wa majirani hao hakuna maana ya kufanya uadui na majirani wengine.

Rais Ilham Aliyev, amedai kwamba zoezi la jeshi la Iran lililofanyika hivi karibuni kwenye mpaka wake na nchi za Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan ni ishara ya uungaji mkono wa Tehran kwa Yerevan.

Akijibu matamshi hayo ya Elham Aliyev, Nasser Kanaani, amesema zoezi hilo la karibuni ni jambo la kawaida kabisa na ambalo lilipangwa siku nyingi nyuma na hata majirani wa Iran kufahamishwa mapema kama ilivyo ada.

Kwa mujibu wa Nasser Kanaani, siasa za msingi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mgogoro wa muda mrefu kati ya majirani wawili wa kaskazini katika eneo la Karabakh daima zimekuwa ni kudumishwa umoja wa ardhi na kupatikana utatuzi wa amani wa mizozo kati ya nchi mbili hizo, kwa kuheshimiwa haki za mataifa hayo na pia kuzingatiwa sheria za kimataifa. Kwa hivyo, Tehran daima imekuwa ikilaani kukaliwa kwa mabavu maeneo ya Jamhuri ya Azerbaijan na kuunga mkono ukombozi wake katika ngazi za juu zaidi za utawala.

Kwa mtazamo wa wataalamu wa masuala ya kisiasa, msimamo wa hivi karibuni wa Rais Ilham Aliyev  wa Jamhuri ya Azerbaijan kuhusu majirani zake ni muhimu kwa kutilia manani masuala kadhaa. Suala la kwanza ni kuwa matamshi hayo ya rais wa Azerbaijan yametolewa katika mazingira ya kuimarishwa mahusiano ya nchi hiyo na utawala haramu wa Israel. Nchi hiyo inadhani kwamba kadiri itakavyochukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndivyo itakavyoimarisha nafasi yake katika siasa za kieneo za utawala wa Kizayuni na Marekani na hivyo kunufaika na msimamo huo.

Suala la pili ni kwamba Ilham Aliyev anajaribu kuonyesha kinyume na ukweli wa mambo, kuwa Armenia inajenga muungano mpya wa kijeshi na nchi jirani, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ili kuimarisha nafasi yake miongoni mwa waungaji mkono wake, ikiwemo Uturuki.

Jalal Mirzai, mtaalamu wa masuala ya kieneo anasema kuhusu jambo hilo kwamba: Hapana shaka kuwa rais wa Azerbaijan anafanya huduma nzuri kwa Wazayuni na waungaji mkono wake wengine ili kustawisha zaidi uhusiano wake na Wamagharibi na Wazayuni.

Suala la tatu ambalo limempelekea Ilham Aliyev kutoa matamshi hayo makali na yasiyo na busara dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni kuwa anafanya juhudi kubwa ili kufidia mapungufu na udhalilishaji ambao amejitakia mwenyewe mbele ya watu wa Azerbaijan katika miaka ya hivi karibuni.

Aliyev anadhani kwamba kwa kujaribu kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ataimarisha msimamo wake mbele ya baadhi ya watu wenye mielekeo ya umagharibi nchini humo na hivyo kuboresha nafasi yake nchini. Hii ni katika hali ambayo wananchi Waislamu wa Azerbaijan wana uelewa wa kutosha kuhusu nia njma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutaka kuimarisha amani na usalama katika eneo, na hasa katika mipaka ya Jamhuri ya Azerbaijan, na kwa hivyo hawatahadaika hata kidogo na propaganda zisizo na msingi dhidi ya serikali ya Tehran.

Kwa vyovyote vile wananchi wa eneo wanajua vyema kwamba urafiki na mahusiano mazuri yanaimarisha usalama wa eneo na hivyo kuleta amani na maendeleo. Ni wazi kuwa maadui hawataki kuona maelewano yakiwepo kati ya Azerbaijan na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kwa msingi huo wanatumia kila fursa ili kuzuia kustawishwa ushirikiano baina ya nchi mbili hizi za Kiislamu.

Kwa msingi huo, watu wa Azerbaijan wanataraji kwamba serikali ya Baku itachukua misimamo ya busara zaidi ambayo itapelekea kuimarishwa misingi ya umoja na mafungamano kati ya nchi za Kiislamu. Hii ni kwa sababu Wazayuni wana wasiwasi mkubwa kuhusu mshikamano wa nchi za Kiislamu ambao wanauona kuwa tishio kubwa kwa uhai wao katika eneo.

342/