Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Novemba 2022

20:43:19
1322196

Onyo la Iran kwa Uingereza kwa vitendo vyake vya kiharibifu humu nchini

Waziri wa Usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katika matukio ya hivi karibuni ya humu nchini, "mkono wa utawala wa Kizayuni katika utekelezaji, mkono wa Uingereza katika propaganda na mkono wa utawala wa kiimla wa Aal Saud katika kugharamia machafuko, imeonekana wazi zaidi."

Hujjatul Islam Sayyid Ismail Khatib amesema hayo na kuongeza kuwa, Iran kamwe haiwezi kuwa kama Uingereza, kuunga mkono vitendo vya kigaidi na kuhatarisha usalama wa nchi nyingine, lakini pia haitoruhusu kabisa kuhatarishwa usalama wake. Hivyo Uingereza itapata majibu mwafaka kutokana na vitendo vyake vya kuchochea machafuko ndani ya Iran.

Waziri wa Usalama wa Iran vile vile amesema, kanali ya televisheni ya lugha ya Kifarsi ya "Iran International" inatambuliwa na vyombo vya usalama vya Iran kuwa ni taasisi ya kigaidi na kuongeza kuwa, wafanyakazi wa kanali hiyo wanasakwa na Wizara ya Usalama ya Iran hivyo mahusiano yoyote na taasisi hiyo ya kigaidi ni sawa na kujiingiza kenye vitendo vya kigaidi na ni tishio kwa usalama wa taifa la Iran. 

Nchi kama Uingereza, Marekani na tawala za kiimla za waitifaki wa madola hayo ya kibeberu katika eneo hili, zimechukuwa misimamo maalumu kufuatia matukio ya hivi karibuni yaliyozusha baadhi ya machafuko katika miji ya Iran, misimamo ambayo imezidi kuonesha kuwa muda wote madola hayo huwa yanasubiri fursa ndogo tu wa kuzidisha mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Iran kwa shabaha ya kufanikisha malengo yao haramu kama vile kuchochea mizozo ya kikabila na kikaumu na kujaribu kuigawa vipande vipande Iran..

Ushahidi wa vyombo vya usalama vya Iran unaonesha wazi kuwa, nchi za Uingereza, Marekani na waitifaki wao katika eneo hili, zimetoa mafunzo maalumu kwa watu wa matabaka tofauti ya Iran kupitia vyombo vya mawasiiano ya umma kwa shabaha ya kuzusha fujo na machafuko ndani ya Iran. Vyombo vya habari vya madola hayo adui ya Magharibi, Kizayuni na Kiarabu tangu zamani vilikuwa vimepanga njama kubwa za kuchochea machafuko hayo na kuyapa nguvu magenge yanayopigania kujitenga kupitia kuchochea hisia za kikaumu na kikabila. Televishheni ya "Iran International" inayoendeshwa na ukoo wa Aal Saud imekuwa mstari wa mbele katika njama hizo. Taasisi hiyo ya kigaidi ya Saudia inarusha matangazo yake kwa uhuru kamili huko Uingereza na kwa msaada wa kila upande wa serikali ya London dhidi ya Iran.

Akihojiwa na Ofisi ya Kuhifadhi na Kusambaza Athari za Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei; waziri wa Usalama wa Iran, Hujjatul Islam Sayyid Ismail Khatib amesema: Mkono wa utawala wa Kizayuni katika utekelezaji, mkono wa Uingereza katika propaganda na mkono wa utawala wa kiimla wa Saudia katika kugharamia machafuko hayo, imeonekana wazi kwenye matukio ya hivi karibuni ya nchini Iran.

Tunaporeja kwenye historia ya Uingereza pia tutaona kuwa, nchi hiyo ya kibeberu imekuwa muda wote ikitumia vyombo vya habari kuingilia masuala ya ndani ya Iran na inang'ang'ania zaidi kwenye kuzusha mizozo na mifarakano kwa shabaha ya kuvuruga mshikamano na umoja wa ardhi ya Iran. Hivi sasa pia, televisheni za lugha ya Kifarsi zillizoko Uingereza kama "Iran International" na "BBC Persia" ndio wahusika wakuu wa machafuko ya ndani ya Iran. Mabanda hayo ya propaganda yanaeneza habari za uongo  na kukuza kupindukia matukio hata madogo madogo yanayohusu Iran na kufundisha waziwazi jinsi ya kufanya machafuko, kuharibu mali za umma na kufanya mauaji ndani ya Iran. Muda wote mabanda hayo ya propaganda ya nchini Uingereza yanajaribu kuonesha kuwa, mfumo wa kisiasa wa nchini Iran utaanguka wakati wowote ule.

Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana taasisi za usalama za Iran zikavihesabu vyombo hivyo vya habari vya nchini Uingereza kuwa ni taasisi za kigaidi na hayo ni kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Mohammad Mahdi Esmaili, Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran naye amtangaza habari ya kufunguliwa katika wizara hiyo, kesi ya kiutaalamu dhidi ya kanali hizo za kigaidi za maadui, zinazoendesha shughuli zao nchini Uingereza. Amesema: Karibuni hivi tutawasilisha mashtaka yetu kwa taasisi za kimataifa. Baadhi ya mashtaka hayo yanahusiana na namna kanali hizo zinavyokanyaga waziwazi misingi ya kazi zao, kama vile kutoa mafunzo rasmi juu ya namna ya kuanzisha machafuko na masuala ya kuwaunga mkono magaidi.