Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Novemba 2022

20:43:57
1322197

Iran yaunda kombora la balestiki la Hypersonic

Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kuzalisha kombora la balestiki la Hypersonic, lenye uwezo wa kupenya mifumo yote ya ngao ya ulinzi wa makombora duniani.

Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh ameyasema hayo leo Alkhamisi pambizoni mwa maadhimisho ya miaka 11, tangu kufariki dunia Hassan Tehrani Moqadam, 'Baba wa sekta ya makombora ya Iran.'

Brigedia Jenerali Hajizadeh ameeleza kuwa, kombora hilo jipya la balestiki la Hypersonic lililoundwa kikamilifu na wataalamu wa Iran, mbali na kuwa na uwezo wa kupenya mifumo ya kisasa ya kutungua makombora, lakini lina uwezo mkubwa wa kupiga shabaha kwa usahihi mkubwa.

Amebainisha kuwa, kombora hilo lina kasi kubwa na uwezo wa aina yake, na kwamba hakuna teknolojia yoyote duniani inayoweza kulitungua hata katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo.

Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa, "Kwa miaka mingi, tumekuwa tukiendeleza shughuli zetu katika anga za mbali chini ya vikwazo shadidi na vya kikatili, lakini  leo hii tumefanikiwa kuzalisha kombora la kisasa kabisa la balestiki la Hypersonic."

Jenerali Hajizadeh ameongeza kuwa, kombora hilo jipya lina uwezo wa kupiga mifumo ya kupambana na makombora ya maadui, na kwamba uzalishaji wake umefungua ukurasa mpya na ni hatua kubwa kuelekea kwenye uzalishaji wa makombora ya kizazi kipya hapa nchini.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa imejiunga na nchi chache duniani zenye teknolojia ya kutengeneza makombora ya aina hiyo ya Hypersonic yenye kasi zaidi ya sauti; ambazo ni Russia, China, Korea Kaskazini na Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, Jumapili iliyopita, Wizara ya Ulinzi ya Iran ilizindua mfumo mpya wa makombora ya kujihami ya masafa marefu ya Bavar (Kujiamini) 373 na pia kulifanyia majarbio kombora jipya la Sayyad B4.

Kabla ya hapo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) lilizindua kwa mafanikio roketi la kubebea satalaiti la Qaem-100 katika anga za mbali. Iran imepiga hatua na kupata mafanikio haya yote katika sekta ya makombora, mifumo ya ulinzi na anga za mbali licha ya vikwazo vya kidhalimu na mashinikizo ya maadui wa taifa hili.

342/