Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Novemba 2022

20:44:31
1322198

Abbas: Haina maana kuwa na nchi ya Palestina bila ya Quds, Gaza na Ukingo wa Magharibi

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza kuwa, haitakuwa na maana yoyote kuwa na nchi ya Palestina bila ya Baitul Muqaddas (Jerusalem), Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Abbas, ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 18 wa kifo cha Yasser Arafat, Rais wa zamani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na akaongeza kuwa: "Hatutakubali kingine chochote ghairi ya nchi ya Palestina itakayokuwa kwenye mipaka ya Juni 4, 1967 na Baitul Muqaddas Mashariki (Jerusalem) ukiwa ndio mji mkuu wake. Hii ndiyo amana aliyotuachia Yasser Arafat na sisi tumeahidi na tumejitolea kuitunza na kuitimiza".Akiwahutubu Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema: "tunayaelewa mateso yenu na tunayahisi mateso yenu katika mzingiro huu wa kidhalimu; na tunajaribu kadiri tuwezavyo kuyapunguza mateso haya, lakini lazima tufahamu kwamba, mateso na maumivu haya yataondoka utakapohitimishwa mpasuko na utengano".

Mahmoud Abbas ameongezea pia kwa kusema: "tofauti hizi zinahatarisha mafanikio ya wananchi wa Palestina, yaliyogharimu kujitoa mhanga kwa Mashahidi, wafungwa na majeruhi".

Itakumbukwa kuwa, Mkutano wa Maridhiano ya Kitaifa baina ya makundi ya Wapalestina ulifanyika tarehe 12 hadi 13 Oktoba katika mji mkuu wa Algeria, Algiers kwa usimamizi wa serikali ya nchi hiyo, na mwishoni mwa mkutano huo wa umoja nchini Algeria, makundi ya Wapalestina yalitia saini kile kilichojulikana kama "Azimio la Algeria kwa ajili ya Umoja wa Kitaifa".../


342/