Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Novemba 2022

20:49:10
1322200

Wapalestina wakosoa njama za Kuyahudisha mtaala wa shule katika jiji la Quds

Wapalestina wanaendelea kulaani vikali njama za utawala haramu wa Israel za Kuyahudisha na kupotosha ukweli katika vitabu vya shule katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Kamati ya Quds ya Baraza la Wananchi la Wapalestina Nje ya Nchi imelaani mitaala potofu ya Israel iliyowekwa kwa ajili ya wanafunzi wa Kipalestina katika mji wa Quds.

Malalamiko hayo yamefuatia usambazaji wa vitabu ambavyo ni pamoja na habari za uwongo kuhusu Palestina na  kupendelea utawala bandia wa  Israeli katika Shule za Al Eman.

Katika taarifa, kamati hiyo imesema kwamba usambazaji wa vitabu hivyo unamaanisha kuwa shule "inashiriki katika mchakato wa Kuyahudisha elimu ya Wapalestina na inakiuka utamaduni wa wanafunzi wa Kipalestina ambao wanafutiliwa mbali ustaarabu wao."

Wazazi wa wanafunzi katika shule hizo wameafikiana na uongozi wa Shule za Al Eman kwamba vitabu vya Israel havitakubaliwa, lakini shule hizo zilikubali mitaala hiyo ya Kiyahudi  kufuatia shinikizo kutoka kwa mamlaka ya uvamizi ya Israel.

Mnamo Julai, utawala haramu wa Israeli ulifuta leseni za shule ambazo zilikataa mitaala yenye kufuata mitaala ya Kiyahudi.

Katika miongo ya karibuni, utawala ghasibu wa Israel umechukua hatua nyingi kwa lengo la kuubadilisha utambulisho wa Kiislamu wa Quds Tukufu hasa kupitia ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kubadilisha mitaala ya shule.

Desemba 23, 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

342/