Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

12 Novemba 2022

20:17:44
1322526

Jitihada za kufunga kituo cha Kiislamu cha Hamburg, Ujerumani

Katika juhudi za madola ya Magharibi za kuunga mkono ghasia na machafuko nchini Iran, vyama vya muungano unaotawala nchini Ujerumani vimetoa wito wa kufungwa Kituo cha Kiislamu na Kiutamduni cha Iran katika mji wa Hamburg nchini humo.

Katika mkondo huo, muungano wa vyama tawala nchini Ujerumani umewasilisha rasimu bungeni ukitaka kufungwa Kituo cha Kiislamu cha Hamburg; na inatazamiwa kuwa Bunge litapigia kura rasimu hiyo na kuchukua uamuzi wa kukifunga au la. Kituo cha Kiislamu cha Hamburg ni miongoni mwa vituo na taasisi muhimu za miaka mingi za Kiislamu nchini Ujerumani; na kiliasisiwa yapata miaka 70 iliyopita na Ayatullahil-Udhma Burujerdi. Miongoni mwa huduma muhimu zinazotolewa na kituo hicho ni pamoja na kuchapisha majarida kwa lugha za Kijerumani na Kifarsi, kutoa huduma za ushauri na elimu na maarifa ya Kislamu. Kituo hicho cha Kiislamu pia kina maktaba yenye zaidi ya vitabu elfu sita vinavyozungumzia maudhui na taaluma tofauti. Kituo hicho kimetoa mchango mkubwa katika kueneza mafundisho sahihi ya Uislamu nchini Ujerumani na kimekuwa eneo muhimu la mikutano na mijumuiko ya Waislamu nchini humo. 

Kutokana na lobi za utawala wa Kizayuni wa Israel na kushika kasi harakati za kundi la kigaidi la MKO nchini Ujerumani; vyombo ya nchi hiyo ya Ulaya vimekuwa vikieneza propaganda chafu dhidi ya kituo hicho cha Kiislamu na kiutamaduni mjini Hamburg. Hujuma hiyo ya kipropaganda na kisiasa imepamba moto zaidi katika miezi miwili ya hivi karibuni sambamba na kuanza ghasia na machafuko katika baadhi ya miji ya Iran. Hasa ikitiliwa maanani kwamba serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya na Marekani zimekuwa zikiunga mkono waziwazi machafuko na ghasia hapa nchini. 

Serikali ya Ujerumani inadai kituo hicho cha kidini kinafanya shughuli zake katika fremu ya siasa na sera za Iran; na kwa msingi huo inadhani kuwa kwa kukifunga kituo hicho itafanikiwa kupunguza moja ya njia za ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini humo. Takwa la kufungwa Kituo cha Kiislamu cha Hamburg ni moja ya vifungu vya mpango wa mada 22 wa vyama vya serikali ya muungano unaotawala Ujerumani dhidi ya Iran; mpango ambao chini ya anwani "Kutetea Haki za Binadamu" umeratibiwa kwa lengo la kuwaunga mkono wafanya fujo na pia kuendeleza machafuko na ghasia nchini Iran. Mpango huo tajwa unataka kuzidishwa vikwazo dhidi ya Iran na kuwaunga mkono wapinzani wa Iran huko Ujerumani. Tangu machafuko yaanze hapa nchini nchi za Magharibi ikiwemo Ujerumani zimewachochea na kuwashajiiisha wafanya fujo sambamba na  kuwawekea vikwazo viongozi mbalimbali wa Iran.  

Jambo muhimu ni hili kwamba, nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani siku zote zinadai eti kuunga mkono uhuru, haki za binadamu na pia uhuru wa kujieleza. Hii ni katika hali ambayo, hatua ya serikali ya muungano tawala wa Ujerumani ya kutaka kukifunga Kituo cha Kiislamu cha mjini Hamburg ambacho kina rekodi safi katika harakarati na shughuli za kidini na kiutamaduni ni mfano wa wazi wa kupinga uhuru wa kujieleza na ni kitendo cha kibaguzi. Aidha vyama vya serikali ya muungano tawala ya Ujerumani vinataka kufungwa Kituo cha Kiislamu cha Hamburg katika hali ambayo takwa hilo linakinzana waziwazi na nara zake za eti kutetea uhuru wa kujieleza huku ikiingilia wazi masuala ya ndani ya Iran na kuunga mkono machafuko na vitendo vya kigaidi nchini Iran na kutaka kuendelezwa matukio hayo.  Bila shaka serikali ya muungano ya Ujerumani haijatosheka na suala hilo hivyo imeazimia kuunga mkono vikwazo zaidi dhidi ya Iran. Kuhusiana na hilo, Annalena Baerbock Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani kwa mara nyingine tena amedhihirisha msimao wa uingiliaji wa nchi hiyo katika masuala ya ndani ya Iran na wakati huo huo kutoa madai ya kuwaunga mkono waibua machafuko. Jumatano iliyopita Baerbock aliandika katika ukurasa wake wa twitter kuwa: Umoja wa Ulaya unafikiria kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran katika kulalamikia kile kinachojdaiwa kuwa kukandamizwa wapinzani nchini humu. Baerbock ameandika kuwa: hatua zinaendelea kuchukuliwa kuhusu majmui ya vikwazo vipya; na tunataka wiki ijayo vikwazo hivyo vitekelezwe." Annalena Baerbock amedai kuwa: "tunafanya jitihada ili kuhakikisha kuwa kinafanyika kikao kuhusu Iran katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa."  

Hatua ya Ujerumani ya kudhihirisha upinzani na chuki yake dhidi ya Iran imekabiliwa na radiamali kali ya Tehran. Iran imezitahadharisha mara kadhaa pande za Ulaya kwamba itakabiliana vikali na uingiliaji wowote katika masuala yake ya ndani. Hossein Amir-Abdullahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika hivi katika ukurasa wake wa twitter: "Bi Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, misimamo ya vitisho, ya uingiliaji kati na isiyo ya kidiplomasia haionyeshi ukomavu na busara. Kitendo cha kuharibu na kuvuruga miunganiko ya siku nyingi kina taathira za muda mrefu. Ujerumani inaweza kuchagua ima maelewano au njia ya makabiliano ili kukabiliana na changamoto za pamoja. Jibu letu litakuwa lenye kufaa na kali." 


342/