Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

12 Novemba 2022

20:18:49
1322528

UN: Nchi zaidi ya 50 ziko katika hatari ya 'kufilisika'

Mkuu wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ameonya kuwa, nchi zaidi ya 50 duniani ziko katika hatari ya kufilisika kutokana na mgogoro wa madeni unaozikabili.

Achim Steiner, Mkuu wa UNDP amesema hayo katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP27 unaofanyika katika mji wa Sharam el-Sheikh nchini Misri, ambapo amesisitiza kuwa mgogoro mkubwa wa madeni umetanda katika nchi 54 duniani.

Steiner ameonya kuwa, iwapo nchi maskini duniani hazitosaidiwa kuondokana na mgogoro wa madeni unaozikabili, basi hazitaweza kukabiliana ipasavyo na mgogoro wa hali ya hewa unaoisakama dunia.

Amefafanua kwa kusema: Kuna nchi 54 katika orodha yetu ya nchi zenye malimbikizi ya madeni, na iwapo migogoro zaidi itaibuka, kiwango cha riba kitaongezeka, gharama za mikopo zitaongezeka zaidi, kutashuhudiwa ongezeko la bei za chakula na nishati, na akthari ya chumi za nchi hizo (54) zitashindwa kulipa madeni yao.  

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, nchi 54 duniani zinahitaji msamaha wa haraka wa madeni ili kuepuka umaskini wa kupindukia na kuzipatia nafasi ya kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa limehimiza udharura wa kuchukuliwa hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufuta madeni, kutoa unafuu zaidi kwa idadi kubwa ya nchi na hata kuongeza vifungu maalumu kwenye mikataba ya dhamana ili kutoa nafasi ya kupumua wakati wa migogoro.

Kwa mujibu Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo UNCTAD, takriban asilimia 60 ya nchi za kipato cha chini barani Afrika hivi sasa ziko kwenye mzigo wa madeni, shinikizo kubwa au katika hatari ya kuingia kwenye madeni huku mamilioni ya Waafrika wakitumbukia tena kwenye umasikini wakati huu wakiwa kwenye hatari kubwa ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

342/