Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

12 Novemba 2022

20:23:44
1322537

Nasrullah: Iran imezishinda tena njama za Marekani na Israel

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amezungumzia machafuko ya hivi karibini nchini Iran na kufeli kwa njama za maadui na kusisitiza kuwa, Kwa mara nyingine tena Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kuzima njama na fitina za Marekani na utawala haramu wa Israel.

Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika maadhimisho ya Siku ya Shahidi yaliyofanyika mjini Beirut. Amesisitiza kuwa, Siku ya Shahidi ni siku ya mashahidi wote kuanzia Bahrain, Palestina, Iran na maeneo mengine ya dunia na kusema, adui Mzayuni amefikia hapa alipo kwa baraka ya damu za mashahidi wa kambi ya mapambano. 

Akizungumzia uchaguzi wa karibuni wa bunge la Israel, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa, hakuna tofauti baina ya Benjamin Netanyahu na Wazayuni wengine, na wote ni watenda jinai na wahalifu. Amesema: "Kwa Hizbullah hakuna tofauti baina ya ushindi wa Netanyahu au Mzayuni mwingine, wote ni wahalifu, ijapokuwa kwamba ushindi wa Netanyahu utazidisha mgawanyiko ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na hapana shaka kwamba kushika madaraka watu wapumbavu huko Israel kutazidisha kasi ya kusambaratika utawala huo."

Sayyid Hassan Nasrullah pia amejibu matamshi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani dhidi ya Lebanon na Hizbullah na kusema: "Marekani ndio msingi wa laana na tauni, na Hizbullah ndiyo iliyoondoa shari na laana ya Marekani nchini Lebanon na kuangamiza tauni hiyo."

Akigusia machafuko ya hivi karibuni nchini Iran na kushindwa maadui kufikia malengo yao, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema: Iran kwa mara nyingine tena imeshinda njama za Marekani na Israel, na nguvu ya nchi hiyo itaongezeka zaidi.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Sayyid Nasrullah amegusia suala la kuchaguliwa rais wa baadaye wa Lebanon na kusema: "Tunataka kujaza pengo katika taasisi hii haraka iwezekanavyo. Hatutaki rais wa kuilinda Hizbullah na muqawama, kwa sababu Hizbullah haihitaji kukingiwa kifua, lakini tunataka rais asiusaliti muqawama na mapambano."

342/