Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

12 Novemba 2022

20:24:23
1322538

Upinzani Bahrain waafikiana kususia uchaguzi wa leo wa Bunge

Vyama na makundi ya upinzani nchini Bahrain yameafikiana kwa kauli moja juu ya kuususia uchaguzi wa Bunge unaotazamiwa kufanyika hii leo nchini humo.

Naibu Katibu Mkuu wa mrengo mkubwa zaidi wa upinzani nchini humo wa al-Wefaq ametangaza kuwa, makundi yote ya upinzani katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi yameafikiana kususia uchaguzi huo wa leo.

Sheikh Hussain al-Daihi, Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Kiislamu cha al-Wefaq ametoa mwito kwa Wabahrain kususia uchaguzi huo wa Bunge, kama ishara ya kuonyesha upinzani wao kwa utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa unaolitawala taifa hilo kwa mkono wa chuma.

Sheikh Daihi ameiambia kanali ya televisheni ya Lualua inayotangaza kwa lugha ya Kiarabu kuwa, "Mamlaka za Bahrain zinajiandaa kufungua ubalozi wa Isral mjini Manama. Ofisi hiyo eti ya kidiplomasia litakuwa pango la ujasusi la utawala wa Tel Aviv, suala ambalo litahatarisha usalama wa Bahrain na eneo zima la Mashariki ya Kati."  

Kabla ya hapo, Sheikh Issa Qassim, kiongozi wa kidini wa mapinduzi ya Bahrain alisema kuwa, kususia uchaguzi huo nchini humo ni hatua inayolenga kulinda demokrasia. Amesisitiza kuwa, madai ya viongozi wa utawala wa Bahrain kwamba, uchaguzi wa leo wa Bunge katika nchi hiyo unalenga kuimarisha demokrasia hayana ukweli na ni urongo mtupu.

Makao makuu ya al-Wefaq iliyopigwa marufuku na Aal-Khalifa

Uchaguzi wa Bunge la Bahrain umepangwa kufanyika leo Novemba 12, huku wanamapinduzi wa nchi hiyo wakiazimia kususia zoezi hilo linalopania kuhalalisha utawala wa kiukoo wa Manama machoni pa dunia.

Tangu Februari 14 mwaka 2011 Bahrain imekumbwa na vuguvugu la harakati za mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa ukoo wa Al Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka kuwa huru, kutekelezwa uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuingia madarakani serikali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. 

342/