Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

12 Novemba 2022

20:24:50
1322539

Mapambo ya uchaguzi wa Bahrain; demokrasia bandia ya ukoo wa Aal-Khalifa

Katika hali ambayo uchaguzi wa bunge la Bahrain umaanza masaa machache yaliyopita, viongozi wa kisiasa na kidini wa nchi hiyo wametoa wito wa kususiwa uchaguzi huo.

Miezi kadhaa iliyopita makundi na vyama mbalimbali vya Bahrain vilitoa wito wa kususiwa uchaguzi huo ambao unafanyika leo Novemba 12. Hasa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita viongozi wa vyama  na makundi mbali mbali yanayopinga utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa, yakiwemo ya kidini, kisiasa, kijamii na kimadhehebu yametoa wito wa kususiwa uchaguzi huo yakisisitiza kuwa ni wa kimaonyesho tu.

Kuna sababu kadhaa tofauti za kutaka uchaguzi huo ususiwe. Sababu ya kwanza inahusiana na malengo ya watawala wa Aal Khalifa ya kuandaa uchaguzi huo wa bunge. Lengo kuu la Aal Khalifa kuandaa uachaguzi huo sio kubuniwa kwa bunge huru na lenye nguvu ya kubuni sheria na kusimamia utendaji wa serikali bali lengo ni kuhalalisha utawala huo. Ni kutokana na ukweli huo ndipo utawala huo ukaamua kuwapa wageni vibali vya kushiriki katika uchaguzi huo, ambapo hiyo inapasa kuwa ni haki ya raia wa Bahrain pakee. Kwa kuzingatia hila hiyo ya wataala wa Bahrain, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema kwamba mipango yote iliyobuniwa na watawala wa Aal Khalifa inalenga kuhalalisha utawala wao na hata wamemwalika Papa wa Kanisa Katoliki kuitemebela nchi hiyo hivi karibuni ili kuandaa uwanja wa kufikia lengo hilo.

Sababu nyingine muhimu ni kwamba kwa mtazamo wa wapinzani wa utawala huo wa kiukoo, uchaguzi huo unachukuliwa na watawala wa Manama kama chombo cha kuimarisha udikteta wao huko Bahrain. Kwa mtazamo wa Sheikh Isa Qassim na wanazuoni wengine  pamoja na viongozi wengi wa kisiasa wa nchi hiyo, uchaguzi unaoandaliwa na watawala wa Aal Khalifa ni mbinu ya kufunga milango ya shughuli za kisiasa na kuongeza mateso na ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kuhusiana na hilo, Sheikh Isa Qassim anasema: "Uchaguzi nchini Bahrain ni njia ya kuimarisha udikteta ambapo raia hutumika kama chombo tu cha kuwezesha utawala kuwadhibiti kikamilifu."

Sababu nyingine ya viongozi wa Bahrain kutaka uchaguzi wa nchi hiyo ususiwe ni kuwa bunge linapasa kuwa tiifu kwa mfalme dhalimu wa nchi hiyo na wala halina uhuru wowote wa kujiamulia mambo bali hutumika tu kama chombo cha kupitisha na kuunga mkono siasa za mfalme. Kwa maelezo hayo na kwa maoni ya sehemu kubwa ya jamii ya Bahrain, bunge kama hilo ambalo hurefusha uhai wake kila baada ya miaka minne ya uchaguzi wa kimaonyesho tu na usio huru, kwa hakika ni mapambo tu ya demokrasia ambayo kutokuwepo kwake hakuna taathira yoyote katika maisha ya watu wa nchi hiyo.

Mojawapo ya sababu zinazoyafanya makundi na vyama vya Bahrain vitoe wito wa kususiwa uchaguzi wa leo ni kwamba uchaguzi huo haujatimiza hata sharti moja la uchaguzi huru, wa wazi na wa haki. Moja ya masharti ya msingi ya uchaguzi huru ni kwamba kila raia aliyetimiza masharti ana haki ya kugombea na kupiga kura. Hii ni katika hali ambayo utawala wa Bahrain umepitisha na kutekeleza sheria ya kuwatenga raia wengi wa nchi hiyo ambapo zaidi ya raia laki moja wamepigwa marufuku kugombea uchaguzi wowote nchini kwao.

Sababu nyingine muhimu ambayo imepelekea kutolewa wito wa kususiwa uchaguzi wa bunge wa Bahrain ni kwamba watawala wa nchi hiyo tangu mwaka 2011 hadi sasa wamekuwa wakiwakandamiza vikali wapinzani na wakosoaji wao. Uchaguzi huweza kuitwa kuwa ni huru hadi pale hali kama hiyo ya ukandamizaji inapoondolewa na kila mtu kuruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi kwa uhuru kamili. Hilo halionekani popote katika chaguzi za Bahrain. Ni wazi kuwa ukandamizaji huo ambao umekuwa ukiendelea nchini kwa zaidi ya muongo mmoja unapaswa kukomeshwa na wananchi kuruhusiwa kuishi katika mazingira huru na tulivu. Katika uwanja huo Said as-Shahabi, Mkuu wa Harakati ya Walio Huru ya Bahrain anasema kwamba uchaguzi wa bunge unaofanyika leo huko Bahrain hautakuwa suluhisho na mgogoro ambao umekuwa ukiendelea nchini humo kwa zaidi ya miaka kumi sasa na wala hautakuwa njia ya kuzima sauti kubwa ya wapinzan wa nchi hiyo.