Main Title

source : Parstoday
Jumapili

13 Novemba 2022

15:54:12
1322832

Mabaharia 16 Wairani waachiliwa huru Tanzania

Mabaharia 16 Wairani waliokuwa wanashikiliwa nchini Tanzania wameachiliwa huru hivi karibuni. Hayo yamedokezwa na Mkuu wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika Eneo la Biashara Huria la Chabahar katika mkoa wa Sistan na Baluchestan kusini-mashariki mwa Iran ambaye amesema mabaharia hao walioachiliwa huru ni wenyeji wa mkoa wa Sistan na Baluchestan.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IQNA, Hassan Karabi mkuu wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika Eneo la Biashara Huria la Chabahar ameongeza kuwa mabaharia hao 16 waliokuwa wanashikiliwa Tanzania wameachiliwa kutokana na ufuatiliaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jijini Dar es Salaam. Aidha taarifa zinasema mabaharia hao walioachiliwa huru waliwasili nchini Iran jana Jumamosi asubuhui.

Hassan Karabi ameongeza kuwa: "Mabaharia walioachiliwa huru walikamatwa na Polisi ya Tanzania takribani miaka 10 iliyopita katika Bahari ya Hindi kwa tuhuma mbali mbali na hadi sasa walikuwa wanashikiliwa gerezani mjini Dar es Salaam."

Mkuu wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika Eneo la Biashara Huria la Chabahar ameendelea kusema kuwa, katika juhudi za kuwasaidia Wairani walio nje ya nchi wanaokabiliwa na matatizo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika safari yake hivi karibuni mjini Dar es Salaam alikutana na viongozi wa ngazi za juu nchini Tanzania na kufanya mazungumzo kuhusu kadhia hii ya mabaharia hao na kuandaa mazingira ambayo yalipelekea waachiliwe huru.


342/