Main Title

source : Parstoday
Jumapili

13 Novemba 2022

15:57:43
1322835

Kilichofanyika Bahrain ni uchaguzi au uteuzi tu wa watu?

Jana Jumamosi, ulifanyika uchaguzi nchini Bahrain wa kuchagua wabunge 40 wa Baraza la Wawakilishi na wajume 30 wa Mabaraza ya Miji.

  Maamuzi yanayopitishwa na bunge hilo la wawakilishi hayana ulazima wa kutekelezwa bali hupata nguvu ya utekelezaji yanapoidhinishwa na bunge la mashauriano inalojulikana kama Seneti, ambalo wajumbe wake wote 40 wanateuliwa na mfalme. Wagombea wote wa uchaguzi walishateuliwa kabla na serikali ya wachache iliyohodhi kila kitu, inayotawala Bahrain. Vyama na makundi ya kisiasa ambayo yanawakilisha wananchi waliowengi yamesusia chaguzi hizo kwa kutaja sababu lukuki, ambapo kwa upande wa harakati ya Al-Wifaq ilitoa taarifa ikitaja karibu sababu 140 zilizoelezea ulazima wa kususia uchaguzi wa jana Jumamosi.

Wakati huo huo, serikali inayotawala Bahrain, kupitia muswada uliopitishwa mwaka 2018, wakati nchi hiyo ilipokuwa ikichukua hatua za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa mashinikizo ya serikali ya Trump na kwa baraka kamili za Saudi Arabia, iliwanyang'anya uraia Wabahrian wengi na kupiga marufuku shughuli za vyama na makundi ya kisiasa ya upinzani, na hivyo kuwanyima haki yao wananchi hao ya kushiriki katika uchaguzi. Sambamba na hatua hiyo, serikali ya Manama iliwapatia uraia, raia wengi wa Kisunni kutoka nchi mbalimbali na hasa wenye imani za kitakfiri ambao walishiriki katika vita vya Syria ili kufanikisha mpango wa kuipindua serikali ya nchi hiyo. Kwa kuwapatia uraia watu hao, utawala wa kifalme wa aila ya Aal Khalifa uliwaandalia mazingira ya kupiga kura katika uchaguzi wa jana.

Kutoa haki ya kupiga kura kwa wanajeshi na kugawanya wilaya za uchaguzi kwa sura ya kikoo ni mbinu na hila nyingine zilizotumiwa na utawala wa Aal Khalifa katika uchaguzi wa jana Jumamosi. Siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi, na kwa mwongozo wa Saudi Arabia, serikali ya Manama iliitisha mkutano wenye kauli mbiu "Mashariki na Magharibi kwa ajili ya Watu Kuishi Pamoja"; na pasi na kumshirikisha kwenye mkutano huo mwakilishi hata mmoja wa raia waliowengi wa nchi hiyo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, iliwaalika shakhsia kama vile Papa Francis na Shekhe wa Al-Azhar ili kwa kufanya hivyo kuipa uhalali hatua yake ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Kizayuni na vilevile kufifisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na itifaki za uchaguzi unaofanyika nchini humo.

Kwa kuzingatia kwamba kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ubaguzi mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Bahrain tangu kuasisiwa kwa nchi hiyo, tunaweza kusema kuwa, moja ya sifa maalumu za uchaguzi bandia wa Novemba 12 ni kuwa kwake uchaguzi wa kwanza kufanyika baada ya utawala wa Aal Khalifa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel; na hiyo ni sababu moja kuu ya ususiaji mkubwa wa uchaguzi huo uliofanywa na vyama na makundi ya wananchi, kama ambavyo kwa sehemu kubwa, utawala wa Manama umefanya kila njia ili kuupatia uhalali wa kisheria uchaguzi huo wa jana kutokana na suala hilohilo la kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala bandia wa Israel.

Ikiwa kabla ya hivi sasa, Saudi Arabia ilikuwa ndiyo yenye sauti ya juu katika upangaji sera za ndani na nje za serikali kibaraka ya Manama, kuanzia sasa, utawala wa Kizayuni nao pia umeongezwa kwenye orodha hiyo; mbali na kwamba Bahrain tokea kuasisiwa kwake imekuwa kituo kikuu pia cha wanajeshi wa Marekani na Uingereza.Laiti kama utawala wa Manama ungelikuwa ni serikali huru inayojitegemea, kungekuwa na uwezekano mkubwa wa kufikiwa suluhu na mwafaka baina yake na wapinzani. Kama ambavyo mchakato huo ulianza baada ya Sheikh Hamad bin Isa Aal Khalifa kuingia madarakani, na ingawa hakutimiza ahadi zake zote kupitia Hati ya Mageuzi ya mwaka 2001, lakini vyama na makundi ya kisiasa ya upinzani yalikubali kufikia maridhiano kwa kupatiwa fursa chache. Na laiti kama mageuzi yaliyoanza mapema mwaka 2000 yangeendelea, huenda wimbi la vuguvugu la wananchi lililojulikana kama Machipuo ya Kiarabu (Arab Spring) lisingefika Bahrain.Hata hivyo, Saudi Arabia, ambayo ndiyo iliyochangia zaidi kuvuruga na kufelisha mpango wa mageuzi ya ndani nchini Bahrain, baada ya kuanza vuguvugu la Machipuo ya Kiarabu, iliingilia kijeshi na kuikalia Bahrain, na kwa kufanya hivyo ikafunga njia zote za kufanyika mageuzi yoyote ya kisiasa ndani ya nchi hiyo; na mkabala wake ikaibebesha mipango yake itakayo, serikali ya wachache yenye uchu wa kuhodhi kila kitu ya ukoo wa Aal Khalifa.

Hivi sasa Bahrain imekuwa tegemezi zaidi kwa Saudi Arabia, na kwa kujiweka karibu na utawala wa Kizayuni, imeathiriwa pia na mielekeo ya utawala huo haramu katika siasa zake za ndani; na ndio maana inaonekana ikiiga na kufuata kikamilifu mbinu zile zile ambazo kwa miongo kadhaa sasa zimekuwa zikitumiwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina, ikiwemo kuwavua uraia wakazi wa asili wa Bahrain na kuwapatia uraia watu ambao hawana asili yoyote ya nchi hiyo.

Katika hali kama hiyo, kufanyika kinachoitwa eti uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi nchini Bahrain si chochote zaidi ya mbwembwe za kisiasa na kipropaganda tu za utawala wa Aal Khalifa na waungaji mkono wake wa nje; na kufanyika uchaguzi huo wa kimaonyesho hakuwezi kubadilisha chochote katika uhalisia wa mambo; na kwa hivyo mazingira ya kushuhudiwa malalamiko na maandamano ya upinzani yataendelea kuwepo.../