Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:38:28
1323351

UN: Idadi ya watu duniani yafika bilioni 8

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa jamii ya watu duniani leo Jumanne Novemba 15 imefikia watu bilioni 8. Kwa mujibu wa makadirio ya umoja huo, hii imetajwa kuwa hatua muhimu katika maendeleo ya mwanadamu kabla ya viwango vya kuzaana kuanza kupungua.

Katika taarifa yake, Umoja wa Mataifa umesema kuwa, idadi hiyo inamaanisha watu bilioni 1 wameongezwa katika  idadi ya watu ulimwengu katika kipindi cha miaka 12 pekee. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, ukuaji huu ambao haujawahi kushuhudiwa umetokana na ongezeko la taratibu la maisha ya binadamu kufuatia kuboreshwa kwa huduma za afya ya umma, lishe, usafi wa mtu binafsi na huduma za matibabu. 

Nchi zenye kipato cha wastani ambazo aghalabu ni za barani Asia zimechangia ukuaji mkubwa katika muongo mmoja uliopita, na hivyo kupelekea ongezeko la takriban watu milioni 700 tangu 2011.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hatua ya kufikia idadi ya watu bilioni 8 duniani ni tukio la kusherehekea kupigwa hatua za kimaendeleo huku tukizingatia uwajibikaji wa pamoja wa binadamu kwa sayari ya dunia. 

Wakati huo huo watalaamu wanasema kuwa, kuwepo idadi kubwa ya watu duniani kunatoa mashinikizo makuu kwa asili ya maumbile ya dunia kwa kuzingatia harakati za ushindani kati ya binadamu na wanyamapori katika vitu kama maji, chakula n.k. 

342/