Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:39:47
1323353

Marekani yaongoza orodha ya nchi zinazofanya israfu ya chakula duniani

Umoja wa Mataifa umesema jamii ya kimataifa haijachukua hatua za maana za kukomesha utupaji wa chakula majaani, huku Marekani, Australia na New Zealand zikiongoza orodha ya nchi zinazofanya israfu kubwa ya chakula duniani.

Rosa Rolle, afisa mwandamizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) amesema mataifa ya dunia yaliahidi mwaka 2015 kupunguza umwagaji wa chakula kwa asilimia 50 kufikia 2030, lakini miaka minane imepita na hakuna hatua za maana zilizopigwa katika uwanja huo.

Amesema hayo katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP27 unaofanyika mjini Sharm el-Sheikh nchini Misri na kuongeza kuwa, mabaki ya chakula yanazalisha ushuri ya gesi zinazosababisha ongezeko la kiwango cha joto la dunia.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, kwa mwaka dunia inafanya israfu kubwa ya chakula kwa kumwaga majalalani tani milioni 931 za mabaki yake. Kwa wastani, kila Mmarekani anatupa jaani kalori 700 za chakula kwa siku, katika hali ambayo anapaswa kula thuluthi moja ya kiwango hicho kwa mujibu wa wataalamu wa lishe na afya.

Kiwango cha kufanya israfu ya chakula nchini Marekani kiliongezeka kwa asilimia 12 kati ya mwaka 2010 na 2016, na hakijawahi kupungua tokea wakati huo. Jean Buzby, afisa wa masuala ya utupaji wa mabaki ya chakula katika Wizara ya Kilimo ya Marekani ameashiria mwenendo wa kusuasua katika kudhibiti umwagaji wa chakula nchini humo na kusema, "Bado tuna safari ndefu ya kufikia malengo (tuliyoyaweka)."

Nchini New Zealand, kiwango hicho cha utupaji wa mabaki ya chakula kimeongezeka hadi asilimia 13.4 mwaka huu, kutoka asilimia 8 mwaka jana. 

Hii ni katika hali ambayo, watu zaidi ya bilioni moja wanateseka kwa baa la njaa na lishe duni katika maeneo mbali mbali duniani. Takwimu za karibuni kabisa za Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, mtu mmoja kati ya kila watu watano barani Afrika anakabiliwa na njaa, huku uhaba wa chakula na utapiamlo ukiongezeka katika bara hilo. 

342/