Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:40:36
1323354

Upinzani wa wananchi wa India dhidi ya safari ya Bin Salman nchini humo

Miji ya New Delhi na Mumbai Jumapili ilishuhudia maandamano makubwa ya wananchi wanaopinga na kulalamikia safari ya Mohammed bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia huko India mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba.

Waandamanaji walikuwa wamebeba vibonzo vya Bin Salman wakilaani mashambulizi ya jeshi la Saudia huko Yemen na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Aal Saudi dhidi ya wapinzani nchini Saudi Arabia. Waandamanaji hao pia wametaka kufutwa safari ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia nchini India. Vilevile walipiga nara wakisema: "Mohammed bin Salman, muuaji na mtenda jinai hana nafasi nchini India". Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia anatarajia kuitembelea India kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Subrahmanyam Jaishankar.

Japokuwa serikali ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, inalipa umuhimu mkubwa suala la kuvutia uwekezaji lakini suala linalopewa uzito na umuhimu zaidi kwa watu wa nchi hiyo ni jinai za kila uchao za Saudi Arabia huko Yemen na mauaji yanayofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Riyadhi dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen. Hii ina maana kwamba, kwa mtazamo wa wananchi wa India, serikali ya nchi hiyo haipasi, kwa gharama yoyote ile, kufanya jitihada za kuvutia uwekezaji wa kigeni kutoka Saudi Arabia na kupuuza haki za binadamu na mikono iliyojaa damu za watu ya Mohammed bin Salman.  

Weledi wa masuala ya kisiasa pia wanatilia maanani jinai zilizotenda na Mohammed bin Salman mwenyewe ikiwa ni pamoja na mauaji ya kinyama ya mwandishi habari aliyekuwa akiukosoa vikali utawala wa ukoo wa Aal Saud, Jamal Khashoggi huko Uturuki. Alaei, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Japokuwa  asili ya Saudi Arabia inafungamana na Uwahabi na serikali ya India imekuwa ikitahadharisha mara kwa mara kuhusu ushawishi wa Uwahabi nchini humo, lakini jinai za Mohammed bin Salman na mauaji yake dhidi ya watu wa Yemen na wapinzani wake vimechafua zaidi jina la Saudi Arabia kote duniani. 

Katika miaka ya hivi karibuni ambapo jina la kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limekuwa likigonga vichwa vya habari; serikali ya India ilikuwa ikihofia pakubwa kuhusu kujipenyeza magaidi wa Kiwahabi na wa Daesh nchini humo. Kwa msingi huo, serikali ya New Delhi iliwaomba msaada wananchi hasa Waislamu wa nchi hiyo ili kuweza kuwatambua na kukabiliana na magaidi; hatua ambayo ilifanikiwa katika uwanja huo. Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, chama tawala BJP hakizingatii masuala ya usalama katika jitihada zake za kuvutia wawekezaji wa kigeni. Wakati huo huo, japokuwa wananchi wa India wanapinga na kudhihirisha malalamiko yao kwa jinai za Bin Salman huko Yemen na kuitaka serikali ya New Delhi kufuta safari ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia, lakini kile kilicho na umuhimu na thamani kwa wananchi wa India ni kuzuia ushawishi wa Saudi Arabia nchini kwao; hatua ambayo bila shaka inaweza kuambatana pia na taathira za kiusalama. 

Surush Amiri mchambuzi wa masuala ya India anasema: "Wananchi wa India bali nchi zote za kusini mashariki mwa Asia daima wamekuwa na wasiwasi za athari mbaya za kiusalama na kuenea itikadi za Kiwahabi kutoka Saudi Arabia. Ni kwa msingi huo ndio maana katika miaka ya hivi karibuni kumechukuliwa hatua kali za kukabiliana na makundi yenye mfungamano na Saudi Arabia katika nchi za Malaysia na Indonesia."  

Ala Kulli hal, maandamano ya wananchi wa India ya kupinga safari ya Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia nchini kwao ni kielelezo cha kugonga mwaba juhudi za Bin Salman za kutaka kusafisha taswira yake ya kigaidi. Vilevile fikra za waliowengi duniani zinaendelea kumtazama Bin Salman kama gaidi ambaye  uwepo wake mahala popote pale unaweza kusababisha taathira zisizoweza kufidiwa. Kwa msingi huo, wananchi wa India wanasisitiza kuwa, serikali ya nchi hiyo haipaswi kupuuza taathira mbaya za safari ya Bin Salman na kujali tu suala la kuvutia wawekezaji kutoka Saudi Arabia kwa gharama yoyote ile.   

342/