Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:41:58
1323356

Vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya na Uingereza dhidi ya Iran; mkinzano wa vitendo na kaulimbiu

Jumatatu ya jana tarehe 14 Novemba, Umoja wa Ulaya na Uingereza zilitangaza kuiwekea vikwazo vipya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hatua iliyopangwa na kuratibiwa baina ya pande mbili hizo.

Uingereza imetangaza kuwaweka katika orodha yake ya vikwazo watu na taasisi 24 za Kiirani kwa kisingizio cha kile kilichoelezwa kuwa kukiuka haki za binadamu. Hatua hiyo ambayo inakiuka dhahir shahidi sheria za kimataifa zinazosisitiza kutoingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine kimsingi inalenga kuwaunga mkono wafanya ghasia na waibua machafuko hapa nchini. Issa Zarepour, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yumo katika orodha hiyo mpya ya shakhsia na asasi zilizowekewa vikwazo.

Umoja wa Ulaya nao kwa upande wake umeongezea katika orodha yake ya vikwazo shakhsai 29 na asasi 3 za Kiirani. Katika orodha hiyo kuna majina manne ya wafanyakazi wa jeshi la polisi, baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na vile vile Brigedia Kiumarsi Haidari kamanda wa jeshi la nchi kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kisingizio kilichotajwa na Umoja wa Ulaya cha kuwawekea vikwazo shakhsia hao ni kukabiliana kwao na wafanya fujo na wavurugaji usalama. Kadhalika Umoja wa Ulaya umeiweka katika orodha yake mpya ya vikwazo Kanali ya Press TV. 

Vikwazo hivyo vinajumuisha marufuku ya kusafiri, kuzuiwa mali za watu na asasi hizo zilizowekewa vikwazo na vilevile marufuku ya mashirika na wananchi wa Ulaya kufanya mabadilishano ya kifedha na asasi na shakhsia hao tajwa. Kwa mujibu wa Umoja wa Ulaya ni kuwa, idadi ya watu na asasi za Kiirani ambazo zimo katika orodha ya vikwazo vya Brussels kwa madai eti ya kukiuka haki za binadamu imeongeza na kufikia watu 126 na asasi 11.

Katika muendelezo wa misimamo ya madola ya Magharibi ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran, Olaf Scholz, Kansela wa Ujerumani sanjari na kuunga mkono fujo na vurugu za Iran amevitaja vitendo vya wafanyafujo na vurugu kuwa ni "mapambano ya kishujaa" na kudai kwamba, vikwazo ni njia ambayo sisi kupitia kwayo tunaongeza mashinikizo dhidi ya Iran.

Kile ambacho kinavuta hisia katika vikwazo hivyo vipya kabla ya kitu kingine chochote ni kuweko katika orodha hiyo Kanali ya Press TV ya lugha ya Kiingereza. Kanali hii ya habari kwa miaka mingi imekuwa ikirusha matangazo yake na kuondoa ukiritimba vya vyombo vya habari vya Magharibi wa kuhodhi mambo ambavyo vimekuwa vikiripot matukio kwa utashi na kwa kupendelea upande fulani sambamba na kulinda maslahi yao. Utendaji wa Kanali ya Press TV ambayo imekuwa ikitangaza ukweli wa mambo na kufichua unafiki na undumakuwili wa vyombo vya habari vya Magharibi katika kutangaza matukio mbalimbali ni jambo ambalo daima limekuwa likiyakasirisha mno madola ya Magharibi, na ndio maana kila baada ya muda fulani yamekuwa yakichukua hatua kama kuifunga kanali hiyo katika mitandao ya kijamii kama Youtube, Instagram na kadhalika. Aidha mashinikizo ya madola hayo mara kadhaa yamezuia kanali hiyo kurusha vipindi vyake katika Satalaiti. 

Filihali pia, madola ya Ulaya yakifuata mkondo wa Marekani ambao ni kinyume kabisa na nara na kaulimbiu ya uhuru wa vyombo vya habari yameiwekea vikwazo Kanali ya Press TV. Hatua hiyo kama yanavyojidanganya madola hayo inalenga  kuzuia kuenezwa mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan kuhusiana na kuweka wazi utambulisho wa wafanyafujo hapa nchini pamoja na nafasi ya madola hayo ya kibeberu katika kuchochea ghasia na vurugu hizo.

Hii ni katika hali ambayo, aina kwa aina ya vyombo vya habari na kanali za televisheni za lugha ya Kifarsi zikipata fedha za madola ya Magharibi na baadhi ya madola yenye fikra mgando katika eneo hili la Asia Magharibvi hususan Saudi Arabia zimekuwa zikifanya kazi zao kwa uhuru kamili huko Ulaya hususan Uingereza licha ya kuendesha uchochezi na propaganda za wazi dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Moja ya kanali hizo za satalaiti ni Iran International ambayo imekuwa ikiendeshwa kwa ufadhili wa kifedha wa Saudi Arabia na ikifuata miongozo ya serikali ya London imekuwa ikieneza anuai kwa anuai za uongo na harakati nyingine haribifu na za kichochezi dhidi ya Iran. Vyombo hivyo vya habari vina uhuru kamili sambamba na kuwaunga mkono wafanyafujo na waibua machafuko nchini Iran. 

Swali la kimsingi hapa hili: Madola ya Ulaya ambayo daima yamekuwa mstari wa mbele kupaza sauti ya kutetea hak za binadamu na kuunga mkono uhuru wa maoni na uhuru wa vyombo vya habari endapo chombo fulani cha habari au kanali fulani ya satalaiti katika mataifa hayo itatangaza habari za kueneza vurugu, machafuko na utumiaji mabavu na kutengeneza silaha za vita yatakuwa tayari kukiruhusu chombo hicho kuendelea kufanya kazi zake kama kawaida? Jibu la swali hilo bila shaka ni hapana. Lakini madola hayo yanaruhusu hilo kwa vyombo vya habari vyenye uadui sugu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran suala ambalo linaweka wazi muendelezo wa uenezaji chuki dhidi ya Iran. Hapana shaka kuwa, hatua hiyo ni mfano na kielelezo cha wazi cha utendaji uleule wa kinafiki na kindumakuwili wa Wamagharibi yakiwemo madola ya Ulaya kuhusiana na masuala kama ugaidi, haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari.


342/