Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:43:45
1323360

Timu ya kandanda ya Iran yawasili Qatar kushiriki Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasili Doha, mji mkuu wa Qatar kwenda kuweka kambi ya kujianjdaa kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza kutifua mavumbi wiki ijayo.

Wachezaji, wakufunzi na benchi la ufundi la timu hiyo imewasili Doha usiku wa kuamkia leo, tayari kwa mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani.

Kabla ya kuelekea Qatar, timu hiyo ilipokewa na kuagwa na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kasri la Rais hapa Tehran.

Rais Raisi amesema uwepo wa timu ya taifa ya soka ya Iran katika mashindano hayo ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) utasaidia kuimarisha umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran, mkabala wa njama za maadui na watu wasiolitakia mema taifa hili.

Rais wa Iran ameitakia kila la kheri timu hiyo akisema kuwa anatumai itajithidi kadri ya uwezo wake kuliletea taifa hili fakhari na heshima, na kutia furaha kwenye nyoyo za Wairani.

Kesho Jumatano timu hiyo ya mpira wa miguu ya Iran inatazamiwa kushuka dimbani kuvaana na Tunisia katika mchuano wake wa mwisho wa kupasha moto misuli. Hivi karibuni ilicheza na Nicaragua hapa nchini na kuigaragaza bao 1-0.

Iran ipo katika Kundi B pamoja na miamba mingine ya soka duniani; Uingereza, Marekani na Wales. Inatazamiwa kuanza kampeni zake Novemba 21, itapochuana na Uingereza, kabla ya kuvaana na Wales Novemba 25, na kisha kupambana mzima mzima na Marekani mnamo Novemba 29.

342/