Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:44:20
1323361

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alaani shambulio la kigaidi la Istanbul Uturuki

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililotokea juzi jioni mjini Istanbul Uturuki na kuua na kujeruhi makumi ya watu.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Uturuki waliopoteza ndugu zao katika tukio hilo la kigaidi na kueleza kwamba, taifa hili linalaani vikali hatua ya kigaidi na kuwauwa watu wasio na hatia yoyote.

Kwa upande wake, Nasser Kan'ani msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran amesema, Tehran inalaani kitendo chochote cha kigaidi ambacho kinahatarisha usalama wa nchi na wananchi wa Uturuki.

Juzi jioni watu 6 waliuawa na wengine 81 walijeruhiwa baada ya kutokea shambulio la kigaidi katika eneo lenye watu wengi la Taksim mjini Istanbul. 

Usiku wa kuamkia jana, Makamu wa Rais wa Uturuki, Fuat Oktay alisema kuwa, mwanamke ndiye aliyefanya shambulio hilo la kigaidi kwa kujiripua kwa mabomu kwenye eneo hilo lenye watu wengi.

Kabla ya hapo, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki naye alikuwa amesema, nchi yake haitotetereshwa na vitendo kama hivyo vya kigaidi.

Aidha alisema katika hotuba yake hiyo ya juzi usiku kwamba, tathmini za awali zinaonesha kuwa shambulio hilo ni la kigaidi.

342/