Main Title

source : Parstoday
Jumatano

16 Novemba 2022

17:17:40
1323736

Rais wa China: Uhuru wa Taiwan na kupatikana amani havitangamani kama maji na moto

Rais Xi Jinping wa China amesema Taiwan kuwa nchi huru na kupatikana amani katika Mlango-Bahari wa kisiwa hicho havitangamani kama yalivyo maji na moto.

Kwa mujibu wa televisheni ya Russia Today, katika matamshi aliyotoa nje ya kikao cha G20, Rais Xi Jinping wa China amesema, suala la Taiwan liko katika orodha ya maslahi makuu na ya msingi ya Beijing na ni msingi wa uhusiano kati ya China na Marekani na akabainisha kwamba: "kadhia ya Taiwan ni mstari wa kwanza mwekundu uliopo katika uhusiano wa Beijing na Washington na haupasi kuvukwa".Xi amesisitiza kwa kusema: "tunatumai kuona amani na uthabiti vinapatikana katika Mlango-Bahari wa Taiwan, lakini "kupatikana suluhu na amani kati ya Taipei na Beijing" na vilevile "uhuru wa Taiwan" ni masuala mawili yasiyoweza kutangamana asilani, kama yalivyo maji na moto.

Aidha, Rais wa China ameeleza matumaini yake kuwa "maneno na matendo ya Marekani yatakuwa kitu kimoja na yatawiana na sera ya China Moja na mikataba mitatu ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Beijing na Washington."

Beijing inaichukulia Taiwan kuwa sehemu isiyoweza kutenganishwa ya ardhi kuu ya China na imeshatahadharisha mara kadhaa dhidi ya uingiliaji wowote wa mambo yake ya ndani au sera ya Magharibi ya kuchochea kujitenga kwa kisiwa hicho.Viongozi wa nchi zinazounda Kundi la G20, zikiwemo China na Marekani jana walianza duru yao ya 17 ya mazungumzo mjini Bali, Indonesia. Katika mkutano huo unaomalizika leo, kuwa na umoja na kuchukua hatua madhubuti za kushughulikia uchumi wa dunia katika kipindi hiki cha vita vya Ukraine, pamoja na masuala yanayohusiana na Taiwan, ni miongoni mwa maudhui zilizojadiliwa na viongozi wa nchi zinazounda kundi hilo la nchi zilizostawi zaidi kiuchumi.../


342/