Main Title

source : Parstoday
Jumatano

16 Novemba 2022

17:19:51
1323740

Wafuasi wa Rais wa Brazil walitaka jeshi kumzuia da Silva kuchukua madaraka

Maelfu ya raia wa Brazil jana walikusanyika nje ya kambi za jeshi jijini Rio de Janeiro, Brasilia na miji mingine Jumanne yakitaka jeshi kuingilia kati kuzuia rais mteule wa mrengo wa kushoto wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva kuchukuwa madaraka mwakani.

Waandamanaji hao walibeba bendera ya Brazil na kuimba wimbo wa taifa na kusisitiza kwamba, hawataki Dal Silva achukue tena madaraka ya nchi.

Wafuasi wa rais anayeondoka madarakani Jair Bolsonaro, ambao bado wana hasira za kushindwa kiongozi wao katiika uchaguzi uliopita, wameshutumu kufanyika udanganyifu katika mifumo ya uchaguzi ambayo imekuwa ikitumika toka mwaka 1996.

Bolsonaro vilevile amekuwa akitoa madai hayo licha ya kutotoa uthibitisho wowote. 

Wizara ya ulinzi ya Brasil, hata hivyo imetoa ripoti kupinga madai hayo ya uchaguzi kuwa na udanganyifu huku waangalizi wa kimataifa pia wakithibitisha uhalali wa uchaguzi.

Rais wa zamani wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva mwishoni mwa mwezi uliopita alimshinda Jair Bolsonaro katika uchaguzi ambao unaashiria kurejea madarakani kwa kishindo kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto.

Ushindi wa da Silva umetajwa kuwa ni kemeo kwa sera za kufurutu ada za mrengo wa kulia ambazo Bolsonaro alikuwa akitekeleza.

Lula da Silva ni kiongozi wa zamani wa chama cha wafanyakazi na alizaliwa katika umaskini. Aliongoza mgomo dhidi ya serikali ya kijeshi ya Brazil katika miaka ya 1970.

342/