Main Title

source : Parstoday
Jumatano

16 Novemba 2022

17:23:48
1323746

Indhari ya UNRWA kuhusu kuongezeka umaskini miongoni mwa wakimbizi wa Kipalestina

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) limetahadharisha kuhusu kuongezeka kwa kiasi kikubwa umaskini miongoni mwa wakimbizi wa Kipalestina huko Syria, Lebanon na Ukanda wa Ghaza.

Wapalestina zaidi ya milioni 6 wanaishi kama wakimbizi katika nchi mbalimbali na hasa katika nchi zinazopakana na Palestina. Wakimbizi hao wa Kipalestina ambao kabla ya kuanza mwamko wa mapinduzi ya wananchi katika nchi za Kiarabu mnamo mwaka 2011 walikuwa wakihesabiwa kama jamii kubwa ya wakimbizi duniani ni zao na natija ya jinai za kila uchao za utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu. Jinai hizo ni pamoja na vita, kuzingirwa ardhi na makazi yao na ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.  

Umoja wa Mataifa ambao umezembea pakubwa mkabala wa jinai za utawala ghasibu wa Israel katika kadhia ya Palestina na kuathiriwa na lobi ya Wazayuni na madola makuu mwezi Disemba mwaka 1949; yaani mwaka mmoja tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Kizayuni uliaanzisha Shirika la Misaada kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). Shirika hilo kama jina lake lilivyowazi lina jukumu la kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina katika nyanja mbalimbali. Shirika hilo linatoa huduma kwa karibu wakimbizi milioni 5 wa Palestina huko Jordan, Syria, Lebanon na katika ardhi zianzokaliwa kwa mabavu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Joradan na pia katika Ukanda wa Ghaza. 

Wakimbizi wa Kipalestina wanakabiliwa na ukosefu wa huduma na suhula muhimu za maisha ikiwemo vifaa vya afya na matibabu. Katika upande wa kiuchumi pia, wakimbizi hao wanakabiliwa na matatizo mengi; ambapo sehemu moja ya matatizo hayo inachangiwa na hatua za jamii ya kimataifa. Kwa mfano, vikwazo dhidi ya Syria vimewasababishia pia matatizo wakimbizi wa Kipalestina au kuendelea vita na mapigano katika nchi kama Syria na Palestina, mgogoro wa kisiasa na kiuchumi huko Lebanon na kuendelea jinai za kila uchao za Israel pia kumechochea pakubwa hali mbaya inayowakabili wakimbizi hao. 

Kuhusiana na suala hili, akizungumza na vyombo vya habari huko Amman mji mkuu wa Jordan Phillippe Lazzarini Mkurugenzi wa shirika la UNRWA ametahadharisha kuhusu kuongezeka pakubwa hali ya umaskini miongoni mwa wakimbizi wa Kipalestina huko Syria, Lebanon na Ghaza na kusema: "hali ya wakimbizi wa Kipalestina walioko Lebanon ni mbaya huku aghalabu yao wakiishi chini ya mstari wa ufakiri. Kiwango cha wastani cha umaskini miongoni mwa wakimbizi hayo kimefikia karibu asilimia 90." Matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wakimbizi wa Kipalestina ni makubwa sana; kama alivyobainisha wazi mkurugenzi wa shirika la UNRWA asilimia 40 ya watoto wa eneo la Ukanda wa Ghaza wanashindwa kupata mlo wa kifungua kinywa. 

Hatua ya serikali ya Marekani ya kukata misaada ya kifedha kwa Shirika hilo la Kuwahudumia Wakimbizi wa Palestina pia ni sababu kuu iliyopelekea hali ya raia hao kuwa mbaya zaidi. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani Agosti mwaka 2018 ilitangaza kusitisha misaada ya kifedha kwa shirika hilo baada ya Palestina kupinga mpango wa kibaguzi wa "Muamala wa Karne."  

Aidha janga la maambukizi ya Corona miaka miwili iliyopita ni sababu nyingine iliyochcohea hali mbaya ya maisha ya wakimbizi wa Kipalestina. Ni wazi kuwa, ugonjwa wa Uviko-10 pamoja na kuzidisha wasiwasi na kutishia afya na usalama wa wakimbizi wa Kipalestina ulikuwa sababu ya kutumbukia katika umaskini idadi kubwa ya raia hao. Hii ni kwa sababu wakimbizi wa Kipalestina pia sawa na matabaka mengine ya raia katika maeneo mengine duniani walipoteza ajira na kazi zao.  

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) limetoa indhari hii kuhusu hali ya umaskini unaowakabili wakimbizi wa Kipalestina ambapo kwa upande mmoja uungaji mkono na misaada ya kimataifa kwa Palestina imepungua; na hata nchi za Magharibi pia zimepunguza misaada yao chini ya kivuli cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni; na katika upande wa pili, kwa kuzingatia kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni, sehemu kubwa ya Wapalestina wanaoishi Ukanda wa Ghaza, Ukingo wa Magharibi na Quds inayokaliwa kwa mabavu pia wameshuhudia kuongezeka matatizo khususan katika sekta za uchumi na afya.    


342/