Main Title

source : Parstoday
Jumatano

16 Novemba 2022

17:24:15
1323747

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan abadilisha msimamo kuhusu Marekani

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan ametoa matamshi yanayotafautiana na msimamo wake wa huko nyuma kuhusu Marekani kwa kusema: "endapo nitashinda uchaguzi, nitahakikisha tunakuwa na uhusiano na Washington utakaotupa izza na heshima".

Khan, kiongozi wa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf na waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, ambaye baada ya kuuzuliwa na bunge amekuwa kila mara akiituhumu Marekani kwamba ilikula njama dhidi yake, ameeleza katika kauli mpya aliyotoa kwamba ana hamu ya kuboresha uhusiano na Washington.

Kuhusu msimamo wake huo wa sasa na tuhuma alizokuwa akitoa dhidi ya Marekani kwamba ilihusika katika njama ya kumwondoa madarakani, Imran Khan ameliambia gazeti la Financial Times kuwa: "kwa upande wangu mimi binafsi, hili limeshamalizika; Pakistan ninayotaka kuiongoza mimi inapasa iwe na uhusiano mzuri na wote, hasa Marekani".

Kiongozi huyo wa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf amesema katika mahojiano na gazeti hilo kuwa, ikiwa atashinda uchaguzi anataka kuwepo na uhusiano wa "heshima" na Marekani na akakosoa uhusiano wa sasa kati ya Washington na Islamabad.

Imran Khan amesema: "uhusiano wetu na Marekani ni mithili ya uhusiano wa bwana na mtumishi au bwana na mtumwa wake; tumekuwa tukitumiwa kama silaha ya kukodi, na kuhusiana na hili, mimi ninahisi serikali za Pakistan zina makosa zaidi kuliko Marekani".

Mbali na kueleza kwamba jeshi la Pakistan haliwezi kutoa "mchango chanya" katika mipango yake juu ya mustakabali wa nchi hiyo, Khan amesisitiza kwa kusema: "inapasa uwepo 'mlingano' katika uhusiano na jeshi na uhusiano na raia".

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan ameeleza bayana: "haiwezekani muwe na serikali iliyochaguliwa, ambayo imeshika madaraka kwa kura za wananchi, lakini wakati huohuo mamlaka yaweko mahali pengine".../

342/