Main Title

source : Parstoday
Jumatano

16 Novemba 2022

17:24:55
1323748

Kurejea Saudi Arabia katika mfumo wa ukandamizaji; sura halisi ya bin Salman

Katika miezi ya hivi karibuni Saudi Arabia imeingia katika hatua mpya ya vitendo vya ukatili na ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa kisiasa, kiraia na wa haki za binadamu.

Viongozi wa utawala vamizi wa Saudi Arabia wameshadidisha utoaji wa hukumu nzito dhidi ya wanaharakati hao na hivyo kuifanya nchi hiyo kuingia katika mkondo mpya wa kushadidisha vitendo vya ukandamizaji.

Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia licha ya kuwa, filihali hana hasimu tishio wa malengo yake ya kukalia kiti cha ufalme wa nchi hiyo, lakini hana kifua cha kuvumilia hata ukosoaji mdogo kabisa dhidi yake. Licha ya wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kiraia nchini Saudia kumekosoa sera za watawala wa Riyadh katika mitandao ya kijamii lakini wametiwa mbaroni na vyombo vya usalama vya nchi hiyo na kuhukumiwa adhabu kali na nzito. Hii inaonyesha kuwa, bin Salman hayuko tayari kuona akikosolewa hata kupitia ibara ndogo tu katika mitandao ya kijamii.

Hivi karibuni mahakama ya Saudia ilimhukumu Salma al-Shahab daktari wa kike na mwanaharakati kifungo cha miaka 35 jela. Noura al-Qahtani ni mwanaharakati mwingine wa kisiasa aliyehukumiwa kifungo cha miaka 45 jela.  Aidha Saudi Arabia imemhukumu kifungo cha miaka 15 jela Mahdiyah al Barzouqi daktari wa kike raia wa Tunisia kwa kuweka tu kwenye ukurasa wake wa Twitter, video ya maandamano ya wananchi wa Tunisia waliokuwa wanaiunga mkono Hizbullah ya Lebanon. Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Kisaudia lenye makao yake barani Ulaya lilifichua hivi karibuni kuwa, viongozi wa Riyadh wamewahukumu adhabu ya kunyongwa wafungwa 15 wa kisiasa wakiwemo watoto kadhaa wadogo. 

Kutolewa hukumu hiyo kunaifanya idadi ya watu wanaokabiliwa na hatima ya kunyongwa kufikia 53 wakiwemo watoto wanane.

Tokea kuanza mwaka huu wa 2022 hadi sasa, Saudi Arabia imewanyonga na kuwatia kitanzi watu wasiopungua 121.

Waidha kesi 81 za watu kunyongwa kwa umati zimeripotiwa nchini humo; hali ambayo inatajwa kuwa mbaya zaidi ya watu kunyongwa kwa umati katika historia. Watu 41 kati ya hao walionyongwa walikuwa wapinzani ambao ni Waislamu wa Madhehebu ya Shia wa nchi hiyo na wenyeji wa maeneo ya Al-Ahsa na Qatif mashariki mwa Saudi Arabia.

Swali la kimsingi linaloulizwa na weledi wa mambo ni kuwa, kwa nini vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa kiraia nchini Saudia kwa mara nyingine tena vimechukua mkondo wa kuongezeka na kuwa wazi zaidi katika siku za hivi karibuni?

Inawezekana kusema kuwa, sababu ya kushadidi ukandamizaji huo inahusiana na dhati ya Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo. Saud al-Saba’ani anaandika katika kitabu chake kimoja kuhusiana na bin Salman: Kuanzia kipindi kile kile cha ubarobaro na kuinukia kwake, kuna vitu viwili vilikuwa vikiunda shakhsia ya Muhammad bin Salman ambavyo ni: Hasira na uchokozi na kwa hakika hivi ndivyo vinavyotilia shaka uaminifu wake. Anaongeza kwa kuandika: Shakhsia ya bin Salman ya kupenda jaha, satwa na ukubwa ni jambo ambalo limemfanya awe na tabia ya ukatili na utumiaji mabavu. 

Ukweli wa mambo ni kuwa, sifa hizi ndizo zilizomfanya bin Salman katika kipindi cha miaka 7 iliyopita apige hatua kwa ajili ya kutwaa kiti cha uongozi wa ngazi ya juu kabisa nchini Saudi Arabia na kuamua kutumia mabavu na ukandamizaji dhidi ya kila mpinzani, mkosoaji na hasimu wake katika njia hiyo na kulifanya hilo kuwa ni katika ajenda zake za wazi na dhahiri kabisa.

Pamoja na hayo, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, vitendo hivyo ima vilipungua au vilikuwa vikitekelezwa kwa siri zaidi. Sababu ya hilo lilitokana na sera pamoja na mtazamo wa Rais Joe Biden wa Marekani kwa Muhammad bin Salman. Biden alimkosoa hadharani bin Salman na hata akatanagza kuwa, kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Saudia ataifanya nchi hiyo itengwe. Kwa muktadha huo, Muhammmad bin Salman ambaye anasubiria kwa hamu kutwaa kiti cha ufalme ameamua kutumia fimbo ya kutembelea katika safari yake hiyo. Hata hivyo safari ya Rais Joe Biden wa Marekani Julai mwaka huu Saudi Arabia na kukutana kwake na bin Salman ilikuwa sawa na kupiga muhuri wa kuhitimisha mashinikizo au kutokuwa na taathira yoyote ukosoaji wa Washington DC kwa Muhammad bin Salman.

Baada ya kumalizika safari hiyo siyo tu kwamba, bin Salman alirejea utendaji wake wa hapo kabla bali alikwenda mbali zaidi kwa kufungua njia ya kutolewa  kutoa hukumu nzito na adhabu kali dhidi ya wanawake wanaharakati wa haki za binadamu wanaoshikiliwa magerezani. Kwa muktadha huo, sababu nyingine ambayo imechangia kushadidi na kuchukua wigo mpana zaidi vitendo vya utumiajia mabavu na ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa kiraia nchini Saudia katika miezi ya hivi karibuni ni kubadilika mwenendo na utendaji wa Biden kwa utawala wa Aal Saud ambao umetenda jinai za kutisha pia huko nchini Yemen.

342/