Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

17 Novemba 2022

18:14:12
1324046

UN: Haijulikani vita kati ya Ukrane na Russia vitamalizika lini

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, hakuna ishara zozote zinazoashiria kufikia ukomo mapigano huko Ukraine.

Miezi 9 ya kujiri vita huko Ukraine inapita sasa huku vita hivyo vikiwa vimesababisha maafa na taathira kubwa za kisiasa, kijeshi, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni; huku nchi za Magharibi zikiendelea kutuma silaha na zana za kivita nchini humo.  

Nchi za Ulaya na hasa Marekani zimezidisha mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Shirikisho la Russia na wakati huo huo zikiendelea kuipatia serikali ya Kiev silaha nyepesi na nzito. Nchi za Magharibi si tu hazijachukua hatua za kuhitimisha vita huko Ukraine bali zimeendelea kuchochea moto wa vita nchini humo.  

Bi Rosemary DiCarlo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumzia suala hilo akisema: ni kweli kwamba hakuna ishara zinazooonyesha kwamba vita Ukraine vinaelekea kumalizika; na upo uwezekano wa kushuhudiwa maafa makubwa madhali vita vingali vinaendelea nchini humo. 

DiCarlo amesema, ameshtushwa na tukio la kuvurumishwa makombora katika ardhi ya Poland karibu na mpaka wa Ukraine na kwamba tukio hilo ni ukumbusho wa kutisha wa kuwepo haja kikamilifu  ya kuzuia kuongezeka vita.  

Radio Zeit ya Poland iliripoti Jumanne jioni kwamba makombora 2 ya Russia yalianguka katika kijiji cha Przewodow katika eneo la Lobelski Voivodeship mashariki mwa Poland kwenye mpaka na Ukraine, na kuua watu wawili. 

Katika upande mwingine, Rais Joe Biden wa Marekani, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, Wizara ya Ulinzi ya Ubelgiji na Rais Andrzej Duda wa Poland wametamka kwa kauli moja kwamba kombora lililotua Poland lilirushwa kutoka mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine.

342/