Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

17 Novemba 2022

18:14:43
1324047

Stoltenberg: Hakuna ishara Russia inapanga kuishambulia NATO

Katibu Mkuu wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) amesema hakuna dalili yoyote inayoashiria kuwa Russia inapanga kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi za NATO.

Jens Stoltenberg alisema hayo jana Jumatano katika kikao na waandishi wa habari, baada ya nchi wanachama wa NATO kufanya mkutano wa mashauriano kwa ombi la Poland, kufuatia 'shambulio' la kombora dhidi ya nchi hiyo ya Ulaya.

Aidha Stoltenberg ameeleza kuwa, mripuko wa kombora uliotokea katika kijiji cha Przewodów mashariki mwa Poland umbali wa kilomita sita kutoka kwenye mpaka wa Ukraine na kuua Wapoland wawili juzi Jumanne, yumkini ulisababishwa na mfumo wa ulinzi wa makombora wa Ukraine.

Hata hivyo anadai kuwa, "licha ya kuwa kombora lilikuwa la Ukraine, lakini (tukio hili) halipaswi kubebeshwa Kiev, na  Russia ndiyo inayobeba dhima kwa kuendeleza vita vyake haramu dhidi ya Ukraine."

Kabla ya hapo pia, Rais wa Poland, Andrzej Sebastian Duda, alifanya kikao cha dharura cha Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyo na kutangaza kwamba: "Hadi sasa hatuna ushahidi wowote kuhusu yalikotokea makombora yaliyopiga ardhi yetu." 

Baada ya kikao cha jana cha nchi wanachama wa NATO, Rais huyo ameachana na mpango wa kutaka kutumiwa Kifungu cha 4 cha Mkataba wa NATO. Kifungu hicho kinasema kwamba, iwapo mmoja wa washirika anaamini kwamba "ardhi, uhuru wa kisiasa au usalama wake unatishiwa," ataidhinisha mchakato wa mashauriano, na nchi zingine wanachama zitashiriki katika uchunguzi.

Kabla ya hapo, vyanzo vya habari vya Magharibi vilijaribu kuuhusisha mripuko huo kombora na Russia na kutaka kuihadaa dunia kwamba, Moscow imeshambulia moja ya nchi wanachama wa NATO.

342/