Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

17 Novemba 2022

18:15:28
1324048

Madai ya shambulio la kombora la Russia dhidi ya Poland: Njama za kuzusha mgogoro mpya wa Magharibi dhidi ya Moscow

Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland imetangaza kuwa: "Siku ya Jumanne alasiri, kombora la jeshi la Russia lilipiga kijiji cha "Przewodów" mashariki mwa Poland kilichoko umbali wa kilomita sita kutoka kwenye mpaka wa Ukraine, na kuua Wapoland wawili."

Vyanzo vya habari vya Magharibi pia vilijaribu kuhusisha shambulizi hilo la makombora na Russia na kutaka kudhihirisha kwamba, Russia imeshambulia moja ya nchi wanachama wa NATO.

Ikijibu madai hayo, Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza Jumanne jioni kwamba ripoti ya vyombo vya habari na maafisa wa Poland kuhusu madai ya shambulizi la makombora la Russia kwenye eneo la Przewodów ni hatua ya uchochezi na ya makusudi yenye lengo la kuzidisha mivutano. Wizara ya Ulinzi ya Russia imesisitiza kuwa: "Hakuna shambulizi la makombora lililofanyika kwenye maeneo ya karibu na mpaka wa Ukraine na Poland." Jumanne iliyopita Russia ilifanya mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya Ukraine kwa kutumia makombora ya cruise.

Kufuatia tukio hilo, Rais wa Poland, Andrzej Sebastian Duda, alifanya kikao cha dharura cha Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyo na kutangaza kwamba: "Hadi sasa hatuna ushahidi wowote kuhusu yalikotokea makombora yaliyopiga ardhi yetu." 

Licha ya matamshi hayo ya Duda, Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland ilimwita na kumsaili balozi wa Ruussia huko Warsaw. 

Wakati huo huo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amedai katika mazungumzo yake ya simu na rais wa Poland kuwa "Ulaya na dunia nzima lazima ilindwe dhidi ya ugaidi wa Russia." Suala hili linaonyesha jinsi Kyiv inavyojaribu kutumia tukio hili  kipropaganda na kisiasa dhidi ya Moscow.

Vyanzo vya kidiplomasia vilitangaza mapema jana Jumatano kwamba mabalozi wa nchi wanachama wa NATO watafanya mkutano wa mashauriano kwa ombi la Poland. Mkutano huo utafanyika baada ya Poland kutangaza kuwa, inafikiria kutumia Kifungu cha 4 cha Mkataba wa NATO. Kifungu cha 4 cha NATO kinasema kwamba, iwapo mmoja wa washirika anaamini kwamba "ardhi, uhuru wa kisiasa au usalama wake unatishiwa," ataidhinisha mchakato wa mashauriano, na nchi zingine wanachama zitashiriki katika uchunguzi. Mashauriano yanayofanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Mkataba wa NATO yanaweza kusababisha hatua ya pamoja ya nchi zote 30 wanachama.

Inaonekana kwamba kuanguka kwa kombora kwenye ardhi ya Poland karibu na mpaka wa nchi hiyo na Ukraine ni tukio kubwa katika mwenendo wa vita nchini Ukraine. Hapo awali maafisa wakuu wa NATO walikuwa wameonya mara kwa mara juu ya jaribio lolote la Ruussia la kushambulia nchi mwanachama wa shirika hilo la kijeshi na kutishia kutoa jibu kali kwa mashambulizi kama hayo. Kwa sasa Poland imekuwa daraja la kupeleka misaada ya kijeshi na silaha za nchi za Magharibi kwa Ukraine, na serikali ya Warsaw imechukua misimamo mikali zaidi dhidi ya Russia.

Ushahidi unaonyesha kuwa, NATO inapanga kutumia madai ya shambulizi la kombora katika ardhi ya Poland kama kisingizio cha kukabiliana moja kwa moja na Russia. Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, hakuna ushahidi wowote wa kuhusika kwa Moscow katika tukio hilo, bali kinyume chake, ushahidi unaonyesha kuwa kombora la mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine, S-300P, lilianguka kwenye ardhi ya Poland na kuua raia wa nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, maafisa wa Marekani wamesema, "matokeo ya awali yanaonyesha kuwa kombora lililopiga Poland lilirushwa na vikosi vya jeshi la Ukraine ili kuzuia makombora ya Russia."

Propaganda za vyombo vya habari vya Magharibi na hatua ya kukurupuka na isiyo na mantiki ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland ya kumwita na kumsaili balozi wa Russia kabla ya kujulikana sababu na mhusika halisi wa tukio hilo, ni ishara ya hamu ya Warsaw ya kuitumbukiza Russia katika makabiliano ya moja kwa moja na NATO.

Ukweli ni kwamba sambamba na kuendelea kwa vita nchini Ukraine na kujiri kwa matukio kama haya ambayo hayaepukiki katika vita, uwezekano wa makabiliano ya moja kwa moja kati ya Russia na NATO umeongezeka zaidi. Mzozo kati ya Russia na NATO unaweza kugeuka haraka na kuwa vita vya upande zote ambavyo vitakuwa na athari mbaya kikanda na kimataifa. Katika mkondo huo ujumbe wa Russia kwenye Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, tukio la Poland ni jaribio la kuzusha mzozo wa moja kwa moja wa kijeshi kati ya NATO na Russia.


342/