Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

17 Novemba 2022

18:19:39
1324056

Israel yatumia bunduki za roboti dhidi ya Wapalestina Ukingo wa Magharibi

Jeshi la utawala haramu wa Israel limepeleka silaha mpya za roboti katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, huku makabiliano baina ya Wazayuni na Wapalestina yakipamba moto.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, Israel imepeleka katika kambi ya wakimbizi ya Al-Aroub mjini al-Khalil (Hebron) eneo la Ukingo wa Magharibi bunduki zinazoendeshwa kwa kitenzambali (rimoti), na zenye uwezo wa kufyatua mabomu ya kutoa machozi, guruneti na risasi za plastiki.

Bunduki hizo za roboti zina kamera pia za kurekodi matukio au kuyarusha moja kwa moja kwenye sava za Wazayuni maghasibu. Wazayuni wanadai kuwa silaha hizo zimepelekwa al-Khalil katika hatua ya majaribio.

Wakazi wa Ukingo wa Magharibi wametiwa wasiwasi na chokochoko hizo mpya za Wazayuni za kuwapelekea bunduki za roboti zinazodhibitiwa kutoka mbali.

Katika miezi ya hivi karibuni, askari makatili wa utawala wa Kizayuni wameshadidisha ukatili na jinai zao dhidi ya Wapalestina hususan katika miji ya Jenin na Nablus eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu.

Hata hivyo wanamuqawama wa Palestina wamejibu mapigo kwa kutekeleza operesheni kadhaa dhidi Wazayuni, ikiwemo ya juzi karibu na kitongoji cha Ariel huko Silfit katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kuangamiza Wazayuni wawili.

Ripoti iliyotolewa mapema mwezi huu wa Novemba na Wizara ya Afya ya Palestina inasema kuwa, Wapalestina zaidi ya 185 wameuawa shahidi na jeshi katili la Israel huko Ukingo wa Magharibi na katika Ukanda wa Gaza tokea mwanzoni mwa mwaka huu 2022.

342/