Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

18 Novemba 2022

19:09:07
1324314

Kan'ani: Kuvifungia vyombo vya habari vya Iran ni uvunjaji wa wazi wa haki za binadamu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran ameonesha hisia zake kuhusu kitendo cha nchi za Magharibi cha kuliwekea vikwazo Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, IRIB.

Nasser Kan'ani Chafi leo Ijumaa ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba kitendo cha nchi za Magharibi cha kuzisaidia na kuzipa maeneo ya kutangazia na uhuru kamili makumi ya kanali na vyombo vya habari vya kigaidi kwa lengo la kulipiga vita taifa la Iran kwa madai ya uhuru wa kusema, lakini wakati huo huo kuipiga marufuku IRIB na televisheni ya Press TV ili kuzuia kufika sauti na misimamo ya Iran kwa walimwengu, kwa hakika ni uvunjaji wa wazi kabisa wa haki za taifa la Iran unaofanywa na nchi za Magharibi ikiwemo Marekani.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, jinai za Marekani dhidi ya mataifa na tawala huru duniani, hazina mwisho. 

Juzi Jumatano pia, Mkuu wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), Peyman Jebeli alisema kuwa, Kanali ya Press TV inaendelea kuendesha shughuli zake kimataifa na kwamba licha ya kukabiliana na washindani wenye nguvu; na licha ya kuwekewa vikwazo vya kila namna, lakini sauti ya Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwafikia walimwengu. 

Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya na Uingereza zilitangaza kuiwekea vikwazo vipya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hatua iliyopangwa na kuratibiwa baina ya pande mbili hizo. Vikwazo hivyo vilivyohusisha shakhsia zaidi ya 20 na asasi kadhaa za Iran vimejumuisha pia kanali ya televisheni ya Press TV. Marekani pia imeiwekea vikwazo IRIB ili kujaribu kuzuia kuwafikia walimwengu sauti ya haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.


342/