Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

18 Novemba 2022

19:15:07
1324322

Kusambaratika miundombinu ya uchumi wa Afghanistan katika miaka 20 ya kukaliwa kwa mabavu na Marekani

Waziri wa Uchumi wa serikali ya wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan amesema kuwa, miaka 20 ya kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na wanajeshi wa Marekani ndio sababu kuu ya kusambaratika miundombinu ya uchumi wa nchi hiyo.

Qari Din Muhammad Hanif ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka 20 cha uwepo wa majeshi vamizi ya Marekani nchini Afghanistan miundomsingi ya uchumi wa nchi hiyo ilipuuzwa na kutelekezwa kabisa, hali ambayo ilipelekea kusambaratika kwake kikamilifu. Waziri huyo wa uchumi wa serikali ya Taliban amesema hayo wakati alipokuwa akielezea hali ya njia za mawasiliano nchini humo pamoja na hali mbaya ya maisha ya wananchi na kusema bayana kwamba, kipindi cha uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan miundombinu ya usafiri na uchukuzi nayo siyo tu kwamba, ilipuuzwa bali hakukuandaliwa mazingira ya chachu za kiuchumi kwa ajili ya uzalishaji.

Kadhalika Waziri wa Uchumi wa Serikali ya Taliban amesema, miaka 20 ya kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na wanajeshi vamizi wa Marekani ilishuhudia kuongeza idadi ya waraibu na watumiaji wa madawa ya kulevya, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizoko, kuna watu milioni 4 hadi milioni 4.5 nchini Afghanistan ambao ni waraibu na watumiaji wa madawa ya kulevya ambayo ni moja ya matokeo mabaya ya kipindi cha kukabiliwa kwa mabavu nchi hiyo na wanajeshi vamizi wa Marekani. 

Matamshi ya Qari Din Muhammad, Waziri wa Uchumi wa serikali ya wanamgambo wa Taliiban kuhusiana na kuangamizwa na Marekani miundombinu ya uchumi ya nchi hiyo ni ukweli ambao unaonyesha kuwa, kwa miongo kadhaa ijayo athari haribifu kwa uchumi wa nchi hiyo zitaendelea kushuhudiwa.

Marekani ilituma wanajeshi nchini Afghanistan baada ya tukio la Septemba 11 na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Katika kipindi cha miaka 20 cha uwepo wa wanajeshi wake pamoja na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO hakuna matunda yaliyopatikana ghairi ya kushadidi ukosefu wa usalama na kusambaratika nchi hiyo katika kila nyanja.

Marekani ilidai kuwa, wakati wa uwepo wa wanajeshi wake nchini Afghanistan sambamba na kuahidi kuangamiza ugaidi na makundi yenye fikra za kuchupa mipaka ilidai itazuia pia ukulima wa mipopi inayozalisha mihadarati ya kasumba na kusafirishwa na kupelekwa katika mataifa mengine. Hii ni katika hali ambayo, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita mbali na kuwa ugaidi haujatokemezwa nchini humo, ukosefu wa usalama na amani nao umekithiri katika nchi hiyo. 

Ripoti mbalimbalii zinatolewa na asasi za kimataifa zinaonyesha kuwa, wakati wa kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na Marekani pamoja na jeshi la NATO, kwa akali uzalishajii wa mihadarati uliongezeka mara nne huku mashamba ya ukulima wa mipopi yakiongezeka mno. Ahadi nyingine tupu ya Marekani ya kupeleka wanajeshi wake nchini Afghanistan na matokeo yake yakawa ni kuuawa maelfu ya watu wasio na hatia ilikuwa ni kurejesha demokkrasia jambo ambalo nalo katu halikutimia kwani hata chaguzi za rais zilizofanyika katika kiindi cha uwepo wa Marekani katika nchi hiyo ziligubikwa na tuhuma za udanganyifu na uchakachuaji wa kura.

Kama vile haitoshi, baada ya Marekani kuondoa wanajeshi wake huko Afghanistan hivi sasa inatekeleza siasa nyingine kama kuzuia mali na fedha za Afghanistan na hivyo kuzidi kuyafanya maisha ya wananchi wa nchi hiyo kuwa magumu siku baada ya siku.

Baada ya Taliban kuingia madarakani nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021, Marekani ilianza kutekeleza sera ya uadui na uhasama dhidi ya kundi hilo. Washington ilizidisha vikwazo dhidi ya Afghanistan na kuzuia dola bilioni kumi ambazo ni mali za benki kuu ya nchi hiyo wakati Waafghani wanaangamia  kwa umasikini na hali mbaya ya uchumi.

Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Afghastan walikuwa wakitaraji kuwa, baada ya Marekani kuondoa wanajeshi wake ingelilipa gharama taifa hilo za  kufidia hasara zilizotokana na vita ambavyo havikuwa na natija yoyote kwao ghairi ya masaibu na maafa. 

 Kila siku kunaripotiwa habari za kuzidi kuwa mbaya hali ya maisha ya wananchii wa Afghanistan. Wizara ya Afya ya Umma ya Afghanistan imetangaza kuwa, 46% ya watu milioni 35 wana matatizo ya kisaikolojia ambapo asilimia 72 kati yao ni wanawake na asilimia 62 ni wanaume.

Dr. Fereidoun Latifi, mtaalamu wa afya ya akili katika Jimbo la Balkh la kaskazini mwa Afghanistan anasema: Inasikitisha kuwa, matatizo ya kiakili yamezidi kuongezeka kutokana na kuongezeka kiwango cha ukosefu wa ajira, kuzorota uchumi na vita vya ndani huko Mazar-i-Sharif na akthari ya watu wanaotaabika ni wanawake na vijana.

Kuhukumiwa wanajeshi wa Marekani waliotenda jinai za kivita nchini Afghanistan, kulipwa fidia familia za wahanga wa vita hivyo na kutolewa gharama za kufidia kwa waathirika wa afya ya akili na ambao wamepata matatizo ya kiroho na kisaikolojia ni miongoni mwa matarajio waliyonayo wananchi wa Afghanistan kutoka kwa Ikulu ya Marekani White House pamoja na washirika wake.

342/