Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

19 Novemba 2022

16:05:53
1324621

Interpol yatoa kibali cha kukamatwa Isabel Dos Santos

Polisi ya Kimataifa, INTERPOL, imetoa kibali cha kimataifa cha kukamatwa kwa bilionea wa Angola na bintiye rais wa zamani wa nchi hiyo Isabel dos Santos.

Shirika la habari la Lusa la Ureno, likinukuu duru rasmi, limesema kibali cha INTERPOL kilitolewa baada ya waendesha mashtaka wa Angola kuliomba shirika hilo "kumtafuta, kumkamata" na kumrejesha dos Santos.

Taarifa zinasema dos Santos (49) anatafutwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya utakatishaji fedha, utapeli na kutumia vibaya mamlaka.

Amekabiliwa na tuhuma za rushwa kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na madai ya Angola mwaka 2020 kwamba yeye na mumewe walikuwa wametoa dola bilioni 1 katika fedha za serikali kwa makampuni ambayo walikuwa na hisa wakati wa urais wa baba yake, ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa ya mafuta ya Sonangol. Isabel dos Santos mara kwa mara amekana kuhusika na makosa hayo.

Kulingana na Lusa, hati ya kukamatwa inasema mfanyabiashara huyo mara nyingi yuko Ureno, Uingereza na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Babake Isabel dos Santos, Jose Eduardo dos Santos, alifariki dunia Julai mwaka huu baada ya kutawala Angola kwa takriban miongo minne hadi 2017.

Wakati mmoja Isabel dos Santos aliwahi kutajwa kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika huku utajiri wake ukikadiriwa kuwa dola bilioni 3.5.

342/