Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

19 Novemba 2022

16:07:54
1324625

Marekani yampa kinga Muhammad bin Salman kwa mauaji ya Khashoggi

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imempa kinga Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ili asishtakiwe kwa mauaji ya Jamal Khashoggi mwandishi habari mkosaji mkuu wa utawala wa Aal Saud. Bin Salman amepewa kinga hiyo licha ya ahadi ya awali ya Rais Joe Biden ya kumwajibisha mtawala huyo wa Saudia kwa jinai hiyo ya kinyama.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imesema: inatambua na kuruhusu kinga hiyo huku ikiashiria mamlaka iliyonayo ya kikatiba na pia sheria ya kijadi ya kimataifa. Imeongeza kuwa, katika kesi hii Waziri Mkuu bin Salman anayo kinga akiwa mamlakani kutoka katika Mahakama hii ya wilaya ya Marekani. 

Itakumbukwa kuwa aliyekuwa mchumba wa Jamal Khashoggi, Hatice Cengiz alikuwa amefungua kesi kuhusu mauaji hayo ya kutisha ya Khashoggi katika mahakama ya wilaya huko Washington DC.

Ilidaiwa kwamba, Khashoggi aliyekuwa raia wa Marekani na mwandishi habari katika gazeti la Washington Post aliteswa, kuuawa na kisha kukatwa vipande vipande kwa amri ya Muhammad bin Salman. Jamal Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul, Uturuki. Aidha Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) awali lilithibitisha kwamba mtawala huyo wa Saudia ndiye aliyehusika na mauaji hayo. 

Mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, Muhammad bin Salman alitangazwa kuwa Waziri Mkuu wa Saudi Arabia katika hatua ambayo weledi wa mambo waliamini kuwa, ilihusishwa na kesi hiyo kwa lengo la kumkinga na hatua zozote za kisheria ambazo zingechukuliwa katika uwanja huo.

342/