Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

19 Novemba 2022

16:09:39
1324628

Haki za taifa la Iran zimekiukwa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya IRIB, Press TV

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani, amelaani uamuzi wa hivi karibuni wa Marekani wa vikwazo vinavyolenga Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na Televisheni ya Press TV akisema ni ukiukaji wa haki za taifa la Iran.

Katika ujumbe kupitia Twitter siku ya Ijumaa, Kan'ani amesema vikwazo vinakuja wakati "vyombo vya habari vya kigaidi" vinavyopinga Iran viko huru kuzua machafuko ndani ya Iran kupitia kampeni yao ya propaganda.

"Kuruhusu mitandao ya kigaidi na vyombo vya habari kufanya maovu dhidi ya taifa la Iran na kuwekea vikwazo IRIB na Press TV ili kuzuia mitazamo ya Iran kufika kote ulimwenguni ni muendelezo wa utawala wa Marekani wa ukiukaji wa wazi wa haki za taifa la Iran," Kan'ani ameandika.

"Hakuna mwisho kwa uhalifu wa baadhi ya nchi dhidi ya mataifa huru na serikali," ameongeza.

Zikichambuliwa kama juhudi zinazolenga kuzuia uhuru wa kusema na mitazamo mbadala, vikwazo hivyo kwa vyombo vya habari vya Iran vimekuja huku Press TV ikiwa imefanikiwa kusambaratisha propaganda na habari feki za vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu ghasia za hivi majuzi nchini.

Vikwazo hivyo vilivyowekwa na Marekani, vinamlenga mkuu wa IRIB Dkt. Peyman Jebeli, mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha habari cha televisheni cha Press TV kinachotumia lugha ya Kiingereza Dkt. Ahmad Norouzi, Makamu Mkurugenzi Mkuu wa IRIB Mohsen Barmahani, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Vipindi vya Press TV Yousef Pour-Anvari pamoja na wanahabari wakuu wa IRIB Ali Rezvani na Ameneh Sadat Zabihpour.

Jumamosi iliyopita pia Umoja wa Ulaya uliweka vikwazo dhidi ya taasisi kadhaa na watu binafsi wa Iran, ikiwa ni pamoja na Press TV, kwa madai ya "ukiukaji wa haki" kufuatia ghasia za hivi majuzi zilizoungwa mkono na mataifa ya kigeni humu nchini.

342/