Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

19 Novemba 2022

16:12:12
1324632

Hujuma tatu za kigaidi katika kipindi cha wiki tatu Iran; adui anatumia ugaidi baada ya kupoteza matumiani katika vita vya kisaikolojia

Katika wiki tatu zilizopita, mashambulizi matatu ya kigaidi yametekelezwa Shiraz, Isfahan na Izeh, miji mitatu ya Iran, ambapo raia 24, ikiwa ni pamoja na wanawake kadhaa na watoto, wameuawa shahidi na makumi ya watu wengine kujeruhiwa.

Siku ya  Jumatano, watu 2 waliokuwa kwenye pikipiki waliwafyatulia risasi watu wa Izeh katika jimbo la Khuzestan na kupelekea watu 7 kuuawa shahidi na wengine 10 kujeruhiwa. Pia, Jumatano jioni, waendesha pikipiki wawili waliwafyatulia risasi maafisa wa usalama huko Isfahan. Katika hujuma hiyo ya kigaidi maafisa watatu wa usalama waliuawa shahidi na mtu mwingine kujeruhiwa. Awali, tarehe 26 Oktoba, katika shambulio la kigaidi la Daesh au ISIS dhidi ya Shahcheragh, kaburi takatifu la Hazrat Ahmed bin Musa (AS), katika mji wa Shiraz, mji mkuu wa Mkoa wa Fars wa Iran, watu 13, wakiwemo watoto 2, waliuawa shahidi huku wengine  30 wakijeruhiwa.

Machafuko nchini Iran yalianza miezi miwili iliyopita. Wafanya ghasia hao ambao wanaungwa mkono na nchi za kigeni, zikiwemo Marekani, Canada, baadhi ya nchi za Ulaya, baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israe, pamoja na baadhi ya makundi ya kigaidi na yanayotaka kujitenga, wamejaribu kila wanaloweza ili kuibua mazingira ya machafuko ya ndani nchini Iran katika miezi miwili iliyopita.

Hali hii ni muendelezo wa sera ya mashinikizo ya juu kabisa iliyoanzishwa mwaka 2018 na serikali ya zamani ya Marekani kwa lengo la kukabiliana na wananchi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tofauti pekee iliyopo ni kwamba kisingizio cha kuibua machafuko na ghasia kimebadilika. Hapo awali, kisingizio kilikuwa uchumi, na wakati huu ni masuala ya kijamii na kiutamaduni.

Baada ya miezi miwili, hali ya kuleta ghasia na machafuko ya ndani imeshindikana kwa sababu ingawa sehemu ndogo ya watu wameonekana barabarani wakipiga nara, lakini watu waliowengi nchini Iran wamegundua kwa busara malengo ya maadui na hivyo wakajitenga na wafanya ghasia. Kwa hiyo, matarajio ya maadui wengi wa kigeni na makundi ya kigaidi na yanayotaka kujitenga ya kuleta machafuko ndani ya Iran yamegonga mwamba. Aidha sehemu kubwa ya wafanyabiashara wa miji tofauti ya Iran wamekataa kufunga biashara zao hata baada ya waibua fujo na ghasia  kuwataka wafanye hivyo. Pamoja na hayo, baadhi walifunga maduka yao nyakati za mchana kwa kuhofia machafuko na ukosefu wa usalama, ili tu kuzuia uharibifu wa mali. Kwa kweli, vita vya kisaikolojia dhidi ya taifa la Iran, ambavyo vimetekelezwa kwa kutumia vyombo vya habari hasa televisheni na mitandao ya kijamiii vimefeli kwa kiwango kikubwa,

Kutokana na kushindwa huko kwa wazi, njama nyingine iliyokuwa imeratibiwa kabla, yaani, matumizi ya ugaidi, imewekwa kwenye ajenda ya maadui ili kuyafanya matukio ya hivi karibuni ndani ya Iran yaingie katika awamu ya matumizi ya silaha. Lakini swali ambalo linaibuka hapa ni kwamba je, ni kwa nini maadui wameamua kutumia ugaidi dhidi ya Iran? Na ni kwa nini wanatekeleza mauaji hayo ya kigaidi?

Moja ya sababu za kugeukia ugaidi ni kuendelea kubakisha hai hali ya machafuko na ukosefu wa usalama katika maeneo tofauti ya Iran. Kwa hivyo, wanawake na watoto pia wanalengwa na magaidi kwa sababu wananchi wengi huathiriwa sana kisaikolojia na kihisia wanapoona wanawake na watoto wanauawa.

Kwa upande mwingine, kutokana na kukaribia kwa Kombe la Dunia la Qatar na ushiriki wa timu ya taifa ya kandanda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashindano hayo, maadui wanatumia  fursa hiyo kuzidisha mashinikizo ya kisaikolojia  dhidi ya timu ya taifa ya Iran ili ifeli katika mechi zake ambazo imepangiwa kucheza na  Uingereza, Marekani na Wales. Hali kadhalika maadui wanaeneza ghasia Iran ili kuchochea fikra za umma duniani dhidi ya  Jamhuri ya Kiislamu  ya Iran.

Sababu nyingine ambayo imewafanya maadui wachochee hujuma za kigaidi Iran ni kufanya mikoa yote ya nchi itumbukie katika ukosefu wa usalama na machafuko. Katika miezi miwili iliyopita, mikoa ya Khuzestan na Isfahan imekuwa na hali ya utulivu na imeathiriwa kidogo sana na vitendo vya ugaidi. Maadui wanalenga hasa kuibua ghasia na machafuko katika mkoa wa Khuzestan kutokana na uwepo wa kaumu au makabila kadhaa katika mkoa huo.

Sababu nyingine ya maadui kugeukia ugaidi ni kufikisha ujumbe huu kwa watu wa Iran kwamba mazingira ya ndani ya Iran si salama kama mamlaka inavyodai. Huu ni mwendelezo wa hali ya vita vya utambuzi. Wakati huo huo, hakuna shaka kuwa kukabiliana na ugaidi na magaidi ni suala gumu kwa nchi zote.

Katika jiji la Istanbul, Uturuki Jumapili iliyopita jioni kulishuhudia mlipuko wa kigaidi, ambapo watu sita waliuawa na wengine 81 kujeruhiwa.

Nukta muhimu ni kwamba, maadui wameweza kutekeleza operesheni za kigaidi huko Izeh na Isfahan, lakini pamoja na hayo Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameweza kusambaratisha njama kadhaa za kutekeleza hujuma za kigaidi katika maeneo mbali mbali ya Iran.

Nukta nyingine tunayoweza kuashiria ni hii kwamba, hujuma za kigaidi za hivi karibuni zilitokea katikati ya mikusanyiko iliyochochewa na wanaopinga mapinduzi. Bila shaka, hivi sasa mikono iliyo nyuma ya pazia katika hujuma za kigaidi na ghasia nchini Iran inazidi kubainika zaidi. Kwa msingi huo  vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vitatoa pigo kubwa kwa magaidi na wale wote wanaowaunga mkono.


342/