Main Title

source : Parstoday
Jumapili

20 Novemba 2022

19:53:36
1324946

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi, COP27, wamalizika Misri kwa mapatano

Baada ya siku kadhaa za mazungumzo makali yaliyoendelea hadi leo Jumapili asubuhi kwa saa za Sharm el-Sheikh, Misri, nchi katika mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP27, zimefikia makubaliano kuhusu matokeo ambayo yameanzisha utaratibu wa ufadhili wa kufidia walioko katika hatari ya 'hasara na uharibifu' kutokana na majanga ya tabianchi yanayosababishwa na wanadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa video uliooneshwa kwenye ukumbi wa mikutano nchini Misri amesema, "COP hii imechukua hatua muhimu kuelekea haki. Ninakaribisha uamuzi wa kuanzisha mfuko wa hasara na uharibifu na kuufanyia kazi katika kipindi kijacho.” Aidha amesisitiza kwamba sauti za wale walio mstari wa mbele katika janga la tabianchi lazima zisikilizwe.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa akirejelea kile ambacho kiliishia kuwa suala gumu zaidi katika COP hii, ikiwa ni mwendelezo wa Mkutano wa kila mwaka wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).

Nchi zinazoendelea zilitoa wito wenye nguvu na unaorudiwa wa kuanzishwa kwa mfuko wa hasara na uharibifu, ili kufidia nchi ambazo ziko hatarini zaidi kwa majanga ya tabianchi, lakini ambazo zimechangia kidogo katika janga la tabianchi. 

"Ni wazi kuwa hii haitatosha, lakini ni ishara ya kisiasa inayohitajika kujenga upya uaminifu uliovunjika," amesema Guterres, huku akisisitiza kwamba mfumo wa Umoja wa Mataifa utaunga mkono juhudi katika kila hatua.

Baada ya kushindwa kufikia muafaka katika muda uliokuwa umepangwa Ijumaa usiku, hatimaye mapema Jumapili wajumbe wameweza kufikia hitimisho juu ya vipengele vigumu zaidi vya ajenda. Hata hivyo, ingawa makubaliano ya ufadhili wa hasara na uharibifu yamekuwa mafanikio kwa walio hatarini, lakini kumekuwa na maendeleo madogo katika COP27 juu ya masuala mengine muhimu yanayohusiana na sababu za ongezeko la joto duniani, hasa juu ya kuondokana na nishati ya mafuta kisukuku na kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto 1.5 za Selsiasi.

342/