Main Title

source : Parstoday
Jumapili

20 Novemba 2022

19:56:12
1324949

Maelfu Mashhad nchini Iran wahudhuria mazishi ya mashahidi watatu waliouawa katika ghasia

Wakazi wa mji wa kaskazini mashariki mwa Iran wa Mashhad wamehudhuria msafara wa mazishi ya wanachama wawili wa kikosi cha kujitolea cha wananchi cha Basij na mwanajeshi mmoja, ambao waliuawa na waasi siku chache zilizopita.

Mazishi hayo ya jana Jumamosi mchana yalivutia umati mkubwa katika mitaa ya Mashhad. Waombolezaji walitembea pamoja na majeneza kuelekea kwenye Haram ya Imam Ridha  AS, Imam wa nane wa madhehebu ya Shia.

Waliohudhuria walipaza sauti kauli mbiu kama vile "Mauti kwa Marekani!" na "Mauti kwa Wanafiki!" kueleza hasira zao dhidi ya maadui wa Uislamu na Jamhuri ya Kiislamu.

Wanachama wa Basij Hossein Zeynalzadeh na Danyal Rezazadeh waliuawa shahidi katika shambulio la visu lililofanywa na wahuni waibua ghasia huko Mashhad siku ya Alhamisi, na mwanajeshi Reza Rezvani aliuawa shahidi katika mji wa kusini-mashariki wa Saravan.

Wengine wanne pia walijeruhiwa katika shambulio la visu huko Mashhad, ambapo wafanya ghasia walijaribu kulazimisha maduka kufungwa kufuatia miito iliyoungwa mkono na madola adui ya kigeni ya kuitisha migomo ya kitaifa nchini Iran, lakini walikabiliwa na upinzani kutoka kwa vikosi vya kujitolea vya Basiji.

Ghasia zinazoungwa mkono na madola hasimu ya Iran zimekumba mikoa mbalimbali ya Iran tangu mwanamke mwenye umri wa miaka 22 Mahsa Amini alipofariki hospitalini Septemba 16, siku tatu baada ya kuanguka katika kituo cha polisi. Uchunguzi umehusisha kifo cha Amini na hali yake ya kiafya kabla ya kukamatwa na hivyo kubatilisha madai kuwa alipigwa na polisi.

Maandamanao ya kulalamikia kifo hicho yalitekwa nyara na maadui ambao waliyageuza kuwa ghasia na fujo na kisha hujuma za kigaidi. Hadi sasa makumi ya raia na maafisa wa usalama wamepoteza maisha katika hujuma hizo za kigaidi. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, magaidi hao wamechoma moto mali ya umma na kuwatesa wanachama kadhaa wa Basij na vikosi vya usalama hadi kufa.

Tarehe 26 Oktoba, gaidi mwenye mafungamano na Daesh alishambulia Haram Takatifu ya Shah Cheragh katika mkoa wa kusini wa Fars kabla ya Sala ya Magharibi na kuwauwa waumini 15 akiwemo mwanamke na watoto wawili na kuwajeruhi wengine 40.

Takriban watu saba pia waliuawa baada ya magaidi kuwafyatulia risasi watu na vikosi vya usalama katika soko lililojaa watu katika jimbo la Khuzestan Izeh siku ya Jumatano jioni. Wizara ya Usalama ya Iran imesema ushahidi umebaini kuwa madola ya Magharibi, hasa Uingereza, Ufaransa na Marekani  na hali kadhalika utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa kifalme wa Saudia ni madola ya kigeni ambayo yanachochea ghasia, machafuko na ugaidi nchini Iran.

342/